Habari

Imewekwa: May, 27 2023

Mkataba wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wasainiwa Simiyu

News Images

Wizara ya Maji imesaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya maji, mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi mkoani Simiyu. Mkataba huu umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandishi Nadhifa Kemikimba na Kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction CooperationCCECC LTD kutoka China ambayo imewakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni hiyo Bw. Wu Zegang.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Mhandisi Kemikimba amesema mradi mzima wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unatarajiwa kugharimu Euro milioni 171 ambazo ni takribani shilingi za Tanzania bilioni 440, lakini mkataba uliosainiwa utahusisha ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji ziwa Victoria kuyapeleka katika maeneo ya wilaya za Busega, Bariadi, Itilima, Meatu na Maswa ambapo gharama za mradi huu zinatarajiwa kuwa euro milioni 64.1 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 166.8.

Amesema mradi huo ukikamilika utawezesha upatikanaji maji kwa asilimia 100 katika miji ya Busega, Bariadi, Lagangabilili, Maswa na Meatu na vijiji vilivyoko pembezoni mwa bomba kuu ambapo wakazi wa maeneo yote hayo wanakadiriwa kufikia 494,000.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb) amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Simiyu kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wanaondokana na changamoto ya huduma ya majisafi na salama. Amesema mkataba unamtaka mkandarasi atekeleze mradi huo kwa miaka minne hadi Agosti 2025, hivyo Wizara itahakikisha inamsimamia kwa ukaribu ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.

Amesisitiza na kuwataka wadau wote wanaohusika katika mradi huo wahakikishe wanashirikiana katika kutekeleza, kusimamia na kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu mradi ili kuleta matokeo chanya.

Fedha za Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Mkoani Simiyu zimechangiwa na wadau mbalimbali ambapo serikali ya Tanzania inatoa Euro milioni 40.7, sawa na shilingi za Tanzania Bilioni 105.8. Serikali ya Ujerumani Euro milioni 26.1 sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 67.9, Shirikika la kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (GCF) Euro milioni 102.7 sawa na shilingi za Tanzania Bilioni 267. Mchango wa wananchi kupitia nguvu zao unatarajiwa kugharimu Euro milioni 1.5 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 3.9