Habari
Waziri Aweso Apokea Mabomba ya Bil. 7, Ataka Mradi wa Maji Mkinga–Horohoro Ukamilike Haraka
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesisitiza kuwa kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mkinga–Horohoro unaotekelezwa katika Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga, ni lazima ikamilike haraka iwezekanavyo na kuzingatia viwango.
Amesema hayo mara baada ya kukagua na kupokea mabomba yenye thamani ya takribani Sh. 7.8 yatakayolazwa zaidi ya km 23 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo wenye lengo la kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi zaidi ya 57,334 wa kata 10 za Mtimbwani, Doda, Mkinga, Manza, Mayomboni, Sigaya, Moa, Duga, na Parungu Kasera, kwenye vijiji 37 vilivyopo pembezoni mwa barabara ya Tanga - Horohoro pamoja na wananchi wa eneo la Horohoro Mpakani
Waziri Aweso amesema pamoja na kuwasili kwa mabomba hayo, amewataka wasimamizi wa mradi huo ambao ni Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA), waweke mikakati madhubuti ya kuhakikisha mkandarasi anakamilisha mradi huo, wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 35.47.
“Niliwaelekeza wataalamu wakati Rais Samia akiweka jiwe la msingi kwenye mradi huu wasisubiri mabomba yote yafike eneo la mradi, bali waendelee na kazi kadiri mabomba yanavyokuwa yanafika ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati,” Aweso amesema.
Amesistiza kuwa mabomba yamefika, ni lazima kazi iliyobaki ikamilike haraka iwezekanavyo. “Nataka ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Januari Kijiji cha Mtimbwani kianze kupata maji na wananchi waanze kunufaika na mradi huu”, Aweso ameelekeza.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amewataka wataalam kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo hata kabla ya mkatba unavyoonesha na kwa ubora.
Utekelezaji wa Mradi wa Mkinga-Horohoro ambao unatumia chanzo cha Maji cha Mto Zigi kupitia Bwawa la Mabayani na Mtambo wa Kusafisha na Kutibu Maji wa Mowe, kwa sasa umefikia asilimia 65 ambapo mabomba yenye urefu wa km 39 yamelazwa na kufukiwa.
Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Februari 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Maji wa Mkinga–Horohoro unaotarajiwa kutatua changamoto kubwa ya ukosefu wa vyanzo vya maji na pia visima kuwa na maji ya chumvi nyingi katika ukanda wa vijiji vya mwambao wa bahari.
Pamoja na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uwepo wa miamba migumu katika eneo la njia ya kupitisha bomba iliyosababisha zoezi la uchimbaji wa mtaro kuwa mgumu na kukwamisha kazi kukamilika kwa muda uliotarajiwa. pamoja na changamoto hizo, mradi unatarajiwa kukamilika tarehe 05 Julai, 2026 kwa mujibu wa mkataba na kuongeza kiwango cha huduma katika Wilaya ya Mkinga kufikia asilimia 88.

