Habari

Imewekwa: Jan, 14 2026

Tanzania na Korea Yafanya Mazungumzo Kutekeleza Mradi wa Maji wa Rufiji

News Images

Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Korea zimefanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Rufiji kama mpango wa muda mrefu wa kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Gridi ya Maji ya Taifa ambapo utatoa maji kutoka kwenye chanzo cha Mto Rufiji na kuyafikisha Dar es Salaam na maeneo jirani kwa ajili ya huduma ya maji.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania, Mhe. Eun Ju Ahn kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo katika Sekta ya Maji kwa kutekleza miradi mbalimbali ya maji nchini.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma, yalijikita katika masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, hususan katika maeneo ya kuimarisha huduma ya majisafi na majitaka, rasilimali za maji pamoja na usalama wa maji, uvunaji wa maji ya mvua pamoja na fursa mpya za uwekezaji katika Sekta ya Maji.

Waziri Aweso amesema kuwa moja ya malengo ya Serikali ni kupata ufumbuzi wa athari ya mabadiliko ya tabianchi zinazochangia ukame na kusababisha changamoto kubwa ya huduma ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam. Amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Rufiji ni hatua muhimu ya kuboresha huduma ya maji jijini Dar es Salaam na maeneo jirani kwa miaka mingi ijayo.

Aidha, Aweso amesema Serikali ya Tanzania na Korea zinashirikiana katika kutekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Majitaka katika Jiji la Dar es Salaam wenye thamani ya takribani Dola za kimarekani milioni 90 unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi wanaokadiriwa kufikia milioni 1.8 katika jiji la Dar es Salaam unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Kupitia utekelezaji wa mradi wa kisasa wa uondoshaji majitaka kwa ujenzi Mtambo wa Kisasa wa Kuchakata Majitaka eneo la Buguruni (maarufu kama Mabwawa ya Majitaka Buguruni) unaotarajiwa kumaliza magonjwa ya mlipuko yalliyokuwa yanawakabili wananchi wa maeneo hayo na kupunguza gharama za uondoshaji wa majitaka kwa wananchi haswa katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Balozi Ahn Eunju amempongeza Waziri Aweso kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Sekta ya Maji pamoja na kufurahishwa na kazi ya utekelezaji wa Mradi wa Majitaka Buguruni. Amesisitiza dhamira ya Korea kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya usalama wa maji ni eneo muhimu la ushirikiano, hususan katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la mahitaji ya huduma za maji.

Pamoja na Mradi wa Majitaka katika Jiji la Dar es Salaam, Serikali za Tanzania na Korea zinatekeleza Mradi wa Majitaka kwa Jijji la Dodoma, Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Salama Vijijini katika mkoa wa Pwani pamoja na mkoa wa Iringa.

Mazungumzo hayo yanadhihirisha dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kufanikisha vipaumbele vya maendeleo ya taifa na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa ajili ya ustawi wa jamii na uchumi wa nchi.