Habari

Imewekwa: Dec, 02 2025

Waziri wa Maji Afanya Ziara ya Nyumba kwa Nyumba Kufuatilia Huduma ya Maji Kinyerezi

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), ametembea nyumba kwa nyumba ili kujua hali halisi ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Kata ya Kinyerezi, wilayani Ilala, Jiji la Dar es Salaam.

Ziara hiyo ililenga kumsaidia Waziri Aweso kujionea uhalisia wa huduma na kusikiliza kero za wananchi wanaohudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika eneo la Dar es Salaam ya Kusini.

Waziri Aweso alitembelea mitaa mbalimbali ya Kinyerezi, kuzungumza na wananchi na pia kufanya mazungumzo na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa.

“Jukumu langu la msingi kama Waziri wa Maji ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Tanzania wanapata huduma ya maji safi, salama na endelevu, na si vinginevyo,” amesema Aweso.

Ametaja kuwa Serikali imewekeza zaidi ya Sh. bilioni 36 katika Mradi wa Maji wa Bangulo, na amesisitiza kwamba wananchi wapatao 70,000 wa Kata ya Kinyerezi, pamoja na Segerea na maeneo jirani, wanapaswa kupata huduma ya maji salama na ya uhakika.

“Maeneo yote yanayopata huduma ya maji, huduma iwe endelevu. Maeneo yasiyo na huduma, tuchambue changamoto zinazozizuia na kuchukua hatua stahiki na za haraka,” amesema Waziri Aweso.

Aidha, Waziri Aweso amebaini kuwa baadhi ya changamoto za huduma ya maji katika Kata ya Kinyerezi zinatokana na uzembe wa baadhi ya watendaji wa DAWASA. Pia, baadhi ya watendaji wanahusiana na biashara ya kinyume cha sheria ya uuzaji wa maji, jambo linalosababisha ukosefu wa maji kwa makusudi.

“Bodi ya DAWASA inapaswa kufanya tathmini ya utendaji wa watendaji wote, ikiwemo mameneja wa mikoa ya huduma ya DAWASA, pamoja na muundo wa taasisi, ili kuboresha usimamizi wa maeneo yao na ufanisi wa majukumu yao,” ameelekeza Waziri Aweso.

Vilevile, amemtaka Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, kuweka kambi maalumu Kinyerezi ili kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi haraka.

Waziri Aweso pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, kuandaa mwongozo wa gharama elekezi za maunganisho ya maji kwa wateja wa mijini na vijijini, ili kumaliza tatizo la tofauti za gharama ambazo ni kero kwa wananchi.

Ziara hii ya Waziri wa Maji na Katibu Mkuu Wizara ya Maji imelenga kumaliza kero za upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo yaliyo pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam.