Habari
Waziri Aweso: Hakuna Kulala Mpaka Tumetimiza Wajibu Wetu kwa Wananchi

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb), ameweka msimamo mzito kwa menejimenti na watendaji wote wa Wizara ya Maji akisisitiza kuwa huu si wakati wa kulegea au kuridhika, bali ni muda wa kufanya kazi kwa bidii, weledi na moyo wa kujituma usiku na mchana kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania.
Akizungumza katika kikao kazi maalum kilichowakutanisha viongozi na watendaji wa Wizara ya Maji kilichofanyika jijini Dodoma, Waziri Aweso alieleza kuwa ni lazima watendaji wote kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwenye Sekta ya Maji kwa kutafuta suluhu za kudumu kwa changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa huduma bora ya maji safi na salama kwa wananchi.
"Hakuna kulala! Huu ni wakati wa kujitolea kikamilifu, kuhakikisha tunalinda heshima ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutekeleza miradi ya maji kwa kasi, ubora na ufanisi wa hali ya juu," alisisitiza Mhe. Aweso.
Ameongeza kuwa azma ya Serikali ni kufikia lengo la kuhakikisha wananchi wa mijini wanapata huduma ya maji kwa kiwango cha asilimia 95 ifikapo mwaka 2025, huku vijijini kiwango hicho kikifikia asilimia 85. Ili kufanikisha malengo hayo. Aidha, Aweso amewataka watendaji wa Wizara kushirikiana kwa karibu, kuwa wabunifu, waaminifu na kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya maji katika ngazi zote.
Katika kikao hicho, Waziri Aweso pia alielekeza menejimenti kuhakikisha kila kiongozi anakuwa sehemu ya suluhisho, si sehemu ya tatizo, na kuhimiza umuhimu wa ufuatiliaji wa mara kwa mara, uwajibikaji, na utoaji wa taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu maendeleo ya miradi ya maji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema kuwa menejimenti ya Wizara imepokea kwa uzito maelekezo hayo na iko tayari kuyatekeleza kwa dhati. Alibainisha kuwa tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha rasilimali fedha, watu na vifaa zinalengwa moja kwa moja katika maeneo yenye changamoto kubwa zaidi ili kuongeza kasi ya utoaji huduma.
“Tunatambua dhamana kubwa tuliyopewa na Taifa. Watendaji wote wa Wizara tumejipanga kuhakikisha tupo mstari wa mbele katika mapinduzi ya sekta ya maji nchini,” alisema Mhandisi Mwajuma.
Kikao hiki ni sehemu ya juhudi endelevu za kuhakikisha Wizara ya Maji inaboresha utendaji kazi wake kwa lengo la kutekeleza kwa ufanisi mpango wa serikali wa kumtua mama ndoo kichwani na kuleta mageuzi ya kweli katika maisha ya wananchi.