Habari

Imewekwa: Jun, 04 2021

Mhe. Aweso Achukua Hatua Kuunusuru Mradi wa Maji Mkoka

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameelekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa aliyekuwa Mhandisi wa Wilaya ya Kongwa, Herbert Kijazi kwa kosa la kutumia zaidi ya Sh. Milioni 600 kutekeleza wa mradi wa maji wa Mkoka katika Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma bila ya kuzingatia ubora wa maji wa chanzo cha mradi huo na kuiingizia hasara Serikali kwa matumizi mabaya ya fedha.

Mhe. Aweso amesikitishwa na maamuzi hayo ambayo yamechangia mradi huo kukosa tija, pamoja na kuisababishia Serikali hasara licha ya taarifa za awali kuonyesha chanzo cha maji cha mradi huo kuwa na chumvi nyingi na kiwango kikubwa cha madini ya fluoride kiafya.

Pia, amewataka Meneja wa Mamlaka ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Dodoma, Dkt. Godfrey Mbabaye pamoja na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kongwa, Mhandisi Kaitaba Lugakingira kuandika barua kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kosa la kuomba fedha kiasi cha Sh. milioni 356 kwa ajili ya kukarabati mradi huo kwa kutumia chanzo hicho hicho chenye changamoto ya ubora wa maji pamoja na kufahamu changamoto hiyo.

Waziri Aweso amewataka wataalam wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) na RUWASA kufanya tathmini ya kina ya mradi huo na kuwasilisha taarifa yake wiki ijayo kabla ya kuidhinisha fedha za ukarabati.

Aidha, ametoa miezi miwili kwa DUWASA kukamilisha kazi ya ujenzi wa mradi wa maji wa Kongwa mjini na kuahidi kutoa zaidi ya Sh. 350 haraka ili uweze kukamilika.

Awali, Waziri Aweso alishiriki zoezi la upandaji miti wa matunda katika eneo la ofisi za Wizara ya Maji, Mtumba ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Mazingira duniani na kuziagiza Bodi za Mabonde zote nchini kutumia maadhimisho hayo kuwaelemisha wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwa dhumuni la kuokoa Ikolojia ili kuwa na vyanzo vya maji endelevu.