Habari
Mbalizi kupata maji Disemba, 2019

Prof. Mbarawa amesema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Mbalizi ambao unatarajia kutoa huduma katika mji huo kwa asilimia 100.
"Nampongeza sana Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mbeya UWASA, Mhandisi Ndele Mengo na timu yake kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa muda mfupi tangu wapewe kazi hii, kwa kweli Mamlaka yenu ni mfano wa kuigwa na Mamlaka zote za maji", Waziri Mbarawa amesema.
Prof. Mbarawa amesema kuwa utekelezaji wa kazi ya ujenzi wa mradi huo inasimamiwa na Mbeya UWASA kwa asilimia 100 na kasi ya ujenzi ni nzuri hali inayodhihirisha wataalam wana uwezo mkubwa wanapoaminiwa na kupewa majukumu makubwa ya utekelezaji wa miradi.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa Mbeya UWASA, Mhandisi Ndele Mengo ameishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuwapa msaada mkubwa katika kila hatua ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mbalizi, huku wakifanikiwa kupunguza gharama zilizokuwa zitumike awali za zaidi ya Shilingi bilioni 5 mpaka takribani Shilingi bilioni 3.
Mhandisi Mengo amesema moja ya mbinu walizotumia ni kutoa elimu na kumuomba kila mwananchi mwenye shamba linapopita bomba kuchimba mtaro kwenye eneo lake na kumlipa gharama za uchimbaji ili kuepuka gharama kubwa za fidia ambazo zingechelewesha mradi na kugharimu fedha nyingi kwenye fidia.
"Mpaka sasa kazi inaenda vizuri na tunatarijia wananchi waanze kupata maji baada ya miezi miwili na kiwango cha huduma kwa asilimia 100," Mhandisi Mengo amesema.
Katika hatua nyingine wakazi wa mji mdogo wa Mbalizi wamesema wamepokea ujenzi wa mradi huo kwa faraja kubwa na kuishukuru Serikali kwa jitihada kubwa ilizochukua katika kuhakikisha inamaliza tatizo la maji.
Mbeya UWASA pamoja na mradi wa Mbalizi, imetekeleza ujenzi wa miradi ya maji ya Masoko, Kapapa na Busokelo iliyokuwa imekwama. Mamlaka nyingine zimetakiwa kwenda Mbeya kujifunza mbinu za ujenzi wa miradi ya maji.
Kitengo cha Mawasiliano