Habari

Imewekwa: Apr, 26 2021

Matumaini ya Vijiji vya Lundo, Lipino, na Ngindo Kupata Maji Yazidi Kuongezeka

News Images

Matumaini ya wananchi wa vijiji vya Lundo, Lipino, na Ngindo katika Wilaya ya Nyasa ya kupata majisafi, salama na yenye kutosheleza yazidi kuongezeka baada ya Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) kufika kukagua utekelezaji wa mradi wa maji utakaosambaza maji katika vijiji vyote vitatu.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lundo Naibu Waziri amesema utekelezaji wa mradi huo unaendelea na amewahakikishia wananchi hao kwamba mradi utakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma ya majisafi na salama na yenye kutosheleza ambayo wameisubiri kwa muda mrefu.

“Nimemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya, Mhandisi Evaristo Ngole kuhakikisha kwamba maeneo ambayo wameshaweka vituo vya kuchotea maji wananchi waanze kupata huduma wakati wanaendelea na kukamilisha utekelezaji wa mradi badala ya wananchi kusubiri mpaka vituo vyote vikamilike”, Mhandisi Mahundi amesema.

Mradi wa pamoja wa Lundo unatekelezwa kwa fedha za Malipo kwa Matokea (P4R) ambapo fedha iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ni zaidi ya Milioni 400 na mradi unatekelezwa kwa kutumia watalaam wa ndani (Force Account).

Pamoja na hayo, Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Nyasa Mhandisi Evaristo Ngole amesema mradi utakapokamilika utahudumia wananchi wapatao 14,070 wa vijiji vya Lundo, Lipingo na Ngido na unatarajiwa kukamilikatarehe 01 Juni, 2021.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi Bi. Hilda Mputa amesema wanaishukuru serikali kwa kuwaletea mradi wa maji ambao utakuwa mkombozi katika vijiji vyao na kuondoa adha ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa sababu wamepata shida ya maji kwa zaidi ya miaka 20.

Kazi ambazo zimeshafanyika katika kutekeleza mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji kwa ajili ya kijiji cha Lundo na Lipingo, ujenzi wa tanki la mita za ujazo 150, ukarabati wa chanzo cha maji na ukarabati wa tanki la mita za ujazo Elfu 30, katika kijiji cha Ngindo, ujenzi wa vituo 38 vya kuchotea maji na ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusambazia maji umbali wa km 24.2.

Kitengo cha Mawasiliano