Habari

Imewekwa: May, 06 2020

Mamlaka za Maji Zaaswa Kutoa Elimu Kuhusu Ankara za Maji

News Images


Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameziasa Mamlaka za Maji nchini kuwekeza katika utoaji elimu ya usomaji wa ankara za maji kwa wateja wake ili kumaliza manung’uniko mengi ya wananchi yanayohusu gharama za matumizi ya maji wanazotozwa kila mwezi.

Naibu Waziri Aweso amesema malalamiko mengi ya wananchi kuhusu malipo ya ankara za maji yanatokana na tabia ya wasomaji mita wengi kushindwa kutoa maelezo ya kina kwa wateja wakati wakisoma mita, na kusababisha wengi wao kuamini gharama wanazotozwa ni kubwa kulinganisha na matumizi yao halisi hata kama ni sahihi kwa kukosa uelewa.

Ametoa kauli baada ya kukagua mradi wa maji Chamwino, ambapo chanzo chake cha maji ni visima vyenye uwezo wa kutoa maji kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Nimebaini tutapunguza malalamiko mengi ya wateja endapo tutaanza utaratibu wa kutoa elimu tunapokuwa tunafika kusoma mita kwenye nyumba za wateja wetu, wengi wao hawana ufahamu na kusababisha mwamko mdogo wa kulipa ankara zao kwa wakati’’, amefafanua Naibu Waziri Aweso.

“Kuanzia sasa mamlaka zetu za maji zihakikishe zinatoa elimu juu ya mita wanazofungia wateja jinsi zinavyofanya kazi, matumizi ya mteja husika na gharama za kila uniti hii itapunguza malalamiko na kutengeneza uaminifu kwa wateja, jambo litakaloongeza utayari wa kulipa ankara zao kwa wakati’’, amesisitiza Naibu Waziri Aweso.

Aidha, Naibu Waziri Aweso amesema wizara itatoa Shilingi Milioni 700 wiki ijayo kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa tenki la maji la ujazo lita milioni 2.5 na ununuzi wa pampu za mradi huo, pamoja na kazi ya ulazaji wa mabomba inayoendelea uweze kukamilika haraka iwezekanavyo.

Mradi huo utagharimu Shilingi milioni 855 kwa awamu ya kwanza na bilioni 1.16 kwa awamu ya pili, una lengo la kuimarisha huduma ya majisafi na majitaka kwa asilimia 95 katika Jiji la Dodoma, Mji wa Chamwino na maeneo ya pembezoni mwa jiji kwa miaka 30 ijayo.