Habari

Imewekwa: Jan, 24 2020

Mamlaka ya Maji Kuanzishwa Rombo

News Images

Kilimanjaro; 24 Januari, 2020

TAARIFA KWA UMMA

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametangaza uamuzi wa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maji katika Halmashauri ya Rombo itakayosimamia utoaji wa huduma ya maji, ikiwa ni sehemu ya kuboresha na kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma maji kwa wakazi wa Halmashauri ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri Aweso amesema kwa kuzingatia ongezeko la mahitaji ya huduma ya maji katika halmasahauri hiyo iundwe mamlaka itakayochukua nafasi ya kampuni ya kijamii ya Kiliwater na kumuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kuanza kwa utaratibu wa kuanzishwa mamlaka itakayosimamia huduma ya maji kwa dhumuni la kumaliza kabisa kero kwa wananchi.

Tangu mwaka 1995 Kampuni ya Kiliwater imekuwa na jukumu la kusimamia utoaji wa huduma ya maji katika mji wa Rombo, hususan uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya maji katika Halmashauri ya Rombo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Aweso ameamuru kukamatwa kwa msimamizi wa kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Shimbi Mashariki, Godson Josea pamoja na mhandisi Amos Thomas wa Kampuni ya HecoSan Mark Ltd yenye kandarasi ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa sababu ya mradi kushindwa kukamilika kwa wakati pamoja na kulipwa fedha na Serikali.

Aidha, ametaka zifuatwe taratibu za kisheria kumuondoa mkandarasi huyo na asilimia 12 ya kazi iliyobaki ifanywe na wataalam wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilayani Rombo. Pia, akimtaka mkandarasi aliyefunga pampu za maji awashe haraka wakati wizara ikifanya utaratibu wa kumlipa pesa alizotakiwa kulipwa na mkandarasi HecoSan Mark Ltd na kusababisha kazi nyingine zisimame.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini