Habari
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan Aweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Mji wa Muheza

Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la mradi wa kuboresha huduma ya majisafi katika Mji wa Muheza wenye thamani ya shilingi bilioni 6.1 utakaomaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mji wa Muheza na vijiji jirani.
Hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi imefanyika Machi 16, 2021 katika kijiji cha Kilapula Wilayani Muheza, Mkoani Tanga na kuhudhuriwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu, Mkurugenzi Msaidizi masuala ya utoaji wa Huduma za Maji, Mhandisi Lydia Joseph akimuwakilisha Katibu Mkuu, Viongozi wa Mkoa wa Tanga na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji.
Ameielekeza Wizara ya Maji kusimamia vyema utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa na huku lengo la kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye mji wa Muheza na vijiji jirani likifikiwa kama ilivyokusudiwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Tanga (Tanga UWASA), Mhandisi Geofrey Hilly mwenye jukumu la usimamizi wa mradi huo alisema kwa muda mrefu Mji wa Muheza umekuwa na uhaba wa maji uliosababishwa na kutokuwepo kwa vyanzo vya maji vya kutosheleza mahitaji.
“Mahitaji ya maji kwa wakazi wa Muheza mjini ni mita za ujazo 5,190 kwa siku ambapo uzalishaji wa maji toka kwenye vyanzo vilivyokuwepo kabla ya mradi huu ni mita za ujazo 1,445 kwa siku,” alisema Mhandisi Hilly.
Alibainisha kwamba kwa kutambua uhaba huo, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais. Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Maji mwaka 2016/17 ilitenga fedha kwa ajili kutekeleza mradi huo kwa lengo la kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mji huo wa Muheza na vijiji jirani.
Uzinduzi wa mradi huo wa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika mji wa Muheza unakwenda sambamba na uzinduzi wa miradi na uwekaji wa jiwe la msingi maeneo mbalimbali kote nchini ikiwa ni kuadhimisha Wiki ya Maji mwaka 2021 inayoanza leo Machi, 16 hadi Machi 22, 2021.
Kitengo cha Mawasiliano