Habari

Imewekwa: Jun, 27 2024

Maabara ya Isotope Dodoma katika utoaji majibu ya maji

News Images

Rais Samia Suluhu Hassan atakumbukwa kwa vizazi vingi hapa nchini kwa kuwezesha maendeleo katika sekta mbalimbali zinazoigusa jamii na uchumi wa nchi. Wadau wa sekta ya maji wataendelea kumkumbuka kwa jinsi alivyopambana na anavyoendelea kupambana kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inamfikia kila Mtanzania. Ameweza kujipambanua kama mama ambaye anafahamu adha wanayopitia akinamama wenzake katika kutafuta huduma ya majisafi.

Rais Samia amefanya maboresho makubwa kwenye maabara ya kukusanya takwimu za maji na kuzifanyia tafiti ili kujua ubora wake kwa matumizi mbalimbali katika jamii, Maabara hii inaitwa ya Isotope iliyoko Jijini Dodoma kwa sasa ni maabara bora na ya kisasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuhusu masuala ya maji. Hatua hii inazidi kuifanya Tanzania kuwa kinara katika maendeleo ya Sekta ya Maji, kuanzia utafiti hadi ujenzi, kama ilivyotambuliwa na Benki ya Dunia kwa ujenzi wa miradi inayotoa huduma kwa wananchi vijijini.

Ahadi ya Chama cha Mapinduzi kupitia ilani iliyokubaliwa na watanzania ambayo inatekelezwa ni kuhakikisha huduma ya majisafi inafikia asilimia 85 vijijini wakati huduma hiyo maeneo ya mijini inafikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025. Bila shaka kila Mtanzania anafahamu na anashuhudia jinsi Rais Samia alivyowezesha huduma hiyo kusambazwa kwa kasi kila kona ya nchi.

Msisitizo wa Rais Samia haukuishia kuhakikisha huduma hiyo inamfikia Mtanzania bila kuzingatia ubora wa huduma hasa katika suala la afya. Kwa sasa Tanzania inazo maabara 17 za ubora wa maji. Maabara saba kati ya hizo zimepata vyeti vya ithibati ambapo zinaweza kufanya kazi kimataifa popote pale na kutambulika . Mipango na kazi inaendelea kuhakikisha maabara zote zinakidhi viwango vya kimataifa.

Rais Samia ameendelea kuwekeza nguvu katika ubora wa vipimo mbalimbali vya sayansi ya maji ambavyo vinaiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi katika masuala mbalimbali ya kitaalam yanayogusa sekta ya maji.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) anasema chini ya utawala wa Rais Samia, serikali imeiweka Wizara ya Maji katika ushirikiano mzuri na mataifa mbalimbali ambayo yameshirikiana na serikali kuiwezesha maabara ya Isotope iliyoko jijini Dodoma kuwa na ubora wa kimataifa.

Anasema huko Nyuma Wizara ya Maji ilikuwa wizara ya kero na lawama kutokana na uwekezaji mdogo, lakini sasa wizara hiyo ina bajeti kubwa. Sehemu mojawapo ambayo imeongezwa nguvu ni bajeti kwa ajili ya kuimarisha maabara hiyo na ya kipekee hapa nchini ambayo sasa ina vifaa vya kisasa na bora kabisa ambavyo vinawezesha kupima ubora wa maji katika Nyanja tofauti tofauti.

Kemia ya kawaida ambayo inapatikana kwenye maabara nyingi Afrika Mashariki na Kati inawezesha kufahamu kiwango cha madini yaitwayo nitrate katika mto, maji chini ya ardhi na udongo. Maarifa hayo ndiyo yanayowawesha kufahamu usalama na ubora wa maji lakini chanzo cha uchafuzi kinajulikana baada uchunguzi kwa kutumia isotope ya nitrate ambayo sasa inapatikana hapa Tanzania kwenye maabara ya Isotope iliyoko Dodoma.

Maabara hiyo imewezeshwa kuwa na vifaa vya kisasa kabisa ambavyo vinaweza kutoa majibu ambayo hayawezi kutiliwa shaka sehemu yoyote Duniani na kwa haraka zaidi. Vifaa hivyo ni kama Liquid Water Isotope Analyser ambayo inaweza kupima sampuli zaidi ya 50 kwa wakati mmoja. Ion Chromtography ambayo licha ya uwezo wake wa kupima sampuli nyingi kwa wakati mmoja, kifaa hiki kina uwezowa kuchambua chembe chembe za madini katika majikama vile anions, cations, chumvi, trace elements na protini na kutengeneza ‘distilled water’.

Hakuna tena ulazima wa kutuma sampuli nje ya nchi isipokuwa nchi za nje zinakaribishwa kuleta sampuli kwenye maabara ya Isotope Dodoma ili kufanyiwa uchunguzi. Hii yote ni mafanikio ya Rais Samia baada ya kuwekeza nguvu na bajeti ya kutosha katika sekta ya maji.

Maeneo ambayo maji yamechafuliwa na mifugo, shughuli za kibinadamu kama madini, kilimo na ujenzi wa miundombinu ya shughuli mbalimbali maabara ya Isotope inatoa majibu na hivyo kuwezesha kufanya maamuzi ikiwemo kuweka miundombinu ya kuzuia uharibifu, pia kuhamisha watu, mifugo au chochote ambacho kitabainika kuwa ndiyo chanzo cha uchafuzi wa maji.

Tofauti na maabara nyingine sasa hivi maabara ya Isotope ina uwezo wa kipekee wa kupima maadiliko ya tabianchi kwa siku za nyuma na hivyo kuwezesha wataalamu na serikali kwa ujumla kutoa mwelekeo wa siku zijazo za mabadiliko ya joto duniani, pia mahitaji ya nishati, upatikanaji wa maji ya kunywa, na vifaa vya kutosha vya chakula.

Maabara ya kisasa ya Isotope ya Dodoma kupitia vifaa vya kisasa kabisa vilivyopo inaenda mbali zaidi kwa kujua jinsi maji juu ya ardhi yanavyovia ardhini na kuhifadhiwa katika miamba inayohifadhi maji chini ya Ardhi (Aquifer). Kujua mahusiano na mwingiliano kati ya Maji chini ya ardhi na juu ya ardhi, na mwenendo wa Maji chini ya ardhi.

Sifa hizi na nyingine nyingi zinaifanya wengi Kutumia lugha rahisi ambayo siyo rasmi kuitambulisha maabara hii kama Carbon 14 ya maji. Sifa hii inatokana na utofauti wake na maabara zingine, pia aina ya kazi zinazofanywa kupitia maabara hii. Moja ya kazi hiyo ni uwezo wake wa kutambua umri wa maji.

Kwa kawaida maji yanapatikana chini ya ardhi na juu ya ardhi. Sehemu kubwa ya maji chini ya ardhi chanzo chake ni juu ya ardhi sababu kuu ikiwa ni mvua. Maji haya huvuja na kujikusanya huko chini, hatimaye kutengeneza chanzo kingine cha maji huko chini. Maabara ya Isotope ya Dodoma ina uwezo mkubwa wa kufahamu ni lini maji hayo yaliyoko chini ya ardhi yalijitenga na yale yaliyoko juu ya ardhi.

Eneo jingine ambalo sasa Wizara ya Maji inajivunia kupitia maabara hiyo ni teknolojia iliyopo kupitia vifaa vya kisasa vinavyoiwezesha kutambua chanzo cha chumvi katika maji chini ya Ardhi iwapo imesababishwa na mwingiliano wa maji ya Bahari, Miyeyuko ya miamba inayopitisha maji au maji yanayovia ardhini na chumvi iliyoyeyuka na kuvukishwa (Evaporation). Pia kufahamu iwapo maji yanavuja kuelekea eneo lolote hasa katika mabwawa ambayo serikali imewekeza gharama kubwa kuyajenga.

Kwa ujumla serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imeupiga mwingi katika maeneo mengi ndani ya sekta ya maji. Maabara ya maji Dodoma inawakaribisha Taasisi za watu Binafsi, serikali, vyuo vikuu Taasisi za Utafiti na hata nchi jirani kuleta sampuli za maji ili kufanyiwa uchunguzi wa kina.