Habari

Imewekwa: Jun, 15 2021

"Lindeni Miundombinu ya Miradi ya Maji” Mhe. Rais Samia

News Images

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kulinda miundombinu ya maji iliyojengwa hapa nchini kwa sababu serikali inaingia gharama kubwa kuitekeleza ili kufikisha huduma ya majisafi katika jamii.

Mhe. Rais Samia amesema hayo mkoani Mwanza wakati akizindua mradi wa maji wa Misungwi wenye thamani ya shilingi bilioni 13.77.

“Naiagiza Wizara na wahandisi wa mkoa na wilaya hapa Mwanza kuhakikisha maji yanasambazwa kwa kasi sana ili yawafikie wananchi wote” Mhe. Rais Samia amesema na kuongeza mazingira yalindwe ili kulinda vyanzo vya maji.

Ameongeza kuwa wananchi wawe na utaratibu wa kuvuna maji ya mvua kwa kujenga mabwawa na visima ili kumaliza tatizo la maji nchini.

Mhe. Rais Samia amewataka wananchi kulipa bili za maji na kuitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) kuto bambikizia wateja bili za maji bali kila mmoja alipe bili kuendana na matumizi halali.

Wakati huhuo, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) katika hafla hiyo amesema kuwa mageuzi yanafanyika katika sekta ya maji ili kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesema mradi wa maji wa Misungwi unauwezo wa kuzalisha lita milioni 4.5 na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi elfu 64, ambapo mradi huo umeongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 42 hadi kufika asilimia 83 kwa eneo la Misungwi mjini. Mradi wa Maji wa Misungwi una mabomba yenye urefu wa kilomita 57.14

Kitengo cha Mawasiliano