Habari

Imewekwa: Feb, 08 2024

Kigoma na mkakati wa kumaliza changamoto ya huduma ya majisafi

News Images

Ndoto na malengo ya viongozi waliopewa dhamana ya kutoa huduma ya maji mkoani Kigoma ni kuhakikisha huduma hiyo inamfikia kila mwananchi Mkoani hapo katika muda uliopangwa.

Hilo ni jukumu la msingi ambalo limewafanya watendaji hao waendelee kuaminika mkoani hapo kwa wanavyopambana kuhakikisha malengo ya serikali yanatimia. Wanasema wanachi wa mkoa huo wakiwemo akina mama wanajituma sana katika shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo kazi za kilimo na biashara. Hivyo, kuwafikishia huduma ya majisafi na salama katika makazi yao kutapunguza eneo moja la kutumia muda mrefu katika maji na kubaki na shughuli na fursa nyingine tele zilizowekwa na serikali za kuongeza kipato.

Eneo la makao makuu ya mkoa huu linahudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA). Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA Poas Kilangi anaishukuru serikali kwa kukamilisha mradi wa Kuboresha Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Kigoma ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya maji katika mji huo, ambapo ziwa Tanganyika ndio chanzo cha maji yaliyochokuliwa eneo la fukwe ya Amani, Kata ya Bangwe.

Kwa upande wa Vijijini huduma ya majisafi inatolewa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ikiongozwa na Meneja wa Mkoa Mhandisi Mathias Mwenda.

Mhandisi Mwenda anasema ushuhuda wa mafanikio ya huduma ya maji katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Kigoma ziko wazi kwa macho ya kila binadamu kwani miradi inaonekana kila kona. Pia ushuhuda uko wazi katika vinywa vya wanufaika kutokana na adha waliyokuwa wakiipata kabla ya kuwezesha huduma hiyo kuwafikia walengwa.

Anakiri kwamba bado kuna changamoto sehemu tofauti tofauti lakini jitihada ziko wazi katika kuhakikisha ndani ya kipindi kilichopangwa huduma hiyo inawafikia wananchi wote. Mhandisi Mwenda akiongea hayo anawaahidi wananchi wa Kigoma wasiwe na shaka au wasiwasi kwasababu serikali inatambua changamoto hiyo na iko mbioni kuitatua kwa kuwaletea faraja.

Anasema eneo analohudumia kuna jumla ya vijiji 306, ambapo vijiji 231 vimeshapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza. Vijiji 30 vina huduma ya maji ambayo bado inafanyiwa kazi ili iwe imara zaidi, wakati vijiji 33 vipo mbioni kupatiwa huduma. Anasema matajarajio ni huduma hiyo kuwafikia wananchi wa vijiji vyote kwa haraka.

Mhandisi Mwenda anarejea kumbukumbu inayompa matumaini kwamba RUWASA ilianzishwa mwaka 2019 wakati huo huduma ya majisafi na salama mkoani hapo ilikuwa ni asilimia 61. Pamoja na hilo, katika miaka minne ya utekelezaji wa kazi, huduma hiyo imepanda hadi kufikia asilimia 70.8 Anafafanua kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa idadi ya miradi 136. Malengo ni kuhakikisha huduma hiyo inasambazwa kwa kila mwananchi wa mkoa wa Kigoma na kwamba uwekezaji unaofanywa na serikali ni mkubwa.

Mhandisi Mwenda anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake wa kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inafanikiwa kila sehemu mkoani hapo. Aidha, anamshukuru Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na timu nzima ya Wizara ya Maji kwa kuwa tayari kuhakikisha ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa mipango hiyo unakwenda vizuri

Anatolea mfano wilaya ya Buhigwe ambayo anakiri ilikuwa moja ya wilaya ambazo zilikuwa na changamoto wakati RUWASA inaanzishwa lakini sasa matumaini ya wananchi yamekuwa makubwa zaidi.

Wilaya hiyo ina jumla ya vijiji 44 ambapo vijiji 30 vina huduma ya majisafi na salama,vijiji 10 vina huduma ya majisafi lakini bado inahitaji kuimarishwa wakati vijiji vinne vipo katika mkakati wa kufikishiwa huduma.

Kwa ujumla huduma ya majisafi katika wilaya hiyo imefikia asilimia 70.2. na vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma vikiwa na matumaini makubwa ya kufikiwa kwa muda mfupi.

Vijiji nane kati ya 10 vyenye huduma ambayo haitoshelezi vipo kwenye mpango na miradi yake ipo katika hatua za utekelezaji kwa ajili ya kupelekewa huduma ya mtandao wa mabomba ya maji, vijijiviwili kati ya vinne ambavyo havina huduma ya maji kabisa vipo katika mpango wa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kuanza kujenga miundombinu ya maji ya bomba. Mipango ni kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na huduma ya majisafi na salama kwa haraka.

Kijijini Migongo katika wilaya ya Buhigwe. John Fransis Mollel ambaye ni Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Buhigwe, anasema kijiji hicho ni moja ya vijiji vilivyokuwa na changamoto kubwa ya maji, na utekelezaji wa mradi wa maji wa Migongo umewezesha eneo hilo kupata huduma ya maji kwa wananchi wote.

Mradi mwingine ambao unatarajiwa kuwa mkombozi katika wilaya hiyo ni mradi wa maji wa Munanila-Nyakimue utakaohudumia vijiji nane ukitajwa ukiwa na thamani ya shilingi bilioni 8.2

Meneja Mollel anasema mradi huo utawezesha huduma ya majisafi kufika asilimia 85 na hivyo kufikia lengo la Serikali la huduma ya maji vijijini kufika asilimia 85 ifikapo mwaka 2025. Anasema nia hasa ni kuhakikisha huduma ya majisafi wilayani Buhigwe inakuwa zaidi ya asilimia 85, pia kuhakikisha akina mama wa Buhigwe wanasahau adha ya huduma ya majisafi, na salama, kwa kufanya kazi nyingine za maendeleo.

Maelezo ya Meneja Mollel yanapata uthibitisho kutoka kwa familia za wanufaika ikiwemo familia ya mzee Bosco Sunzu Njinyari wa Kijiji cha Migongo. Mzee Njinyari anaishukuru serikali kwa kutekeleza mradi wa maji wa Migongo.Anasema mradi huo umembadilisha kiuchumi kwani umemuwezesha kuimarisha shughuli ya ufugaji ikiwamo wa kuku, bata na mbuzi mifugo ambayo inamuingizia kipato. Pia amekuwa mkulima mzuri kwani anaotesha miche ya bustani katika makazi yake karibu na eneo la Bomba. Miche hiyo inahamishwa kupelekwa mashambani na hatimaye kuongeza mapato ya kilimo.

Wanufaika wengine wa huduma ya majisafi katika Kijiji hiki ni Emakulata Deodatus. Anasema amejikomboa kwa kiasi kikubwa baada ya kupata huduma ya maji. Anasema usumbufu ulikuwa mkubwa kutokana na asili ya eneo hilo lenye miinuko na mabonde. Emakulata anaongeza kuwa sasa hali ni nzuri, usafi umeongezeka, usumbufu umeisha.

Mwingine ni Dules Manase ambaye anashuhuda ya adha ya kuamka saa 12 kwenda mabondeni kutafuta huduma ya maji. Anakiri kwamba maji hayana mbadala hivyo kinachoendelea sasa ni shukrani kwa serikali inayoongozwa na Rais Samia suluhu Hassan. Hawakuwa na uwezo wa kutunza bustani kipindi cha kiangazi lakini sasa inawezekana.

Mkazi mwingine Bi. Veronica Chuma anasema huduma ya maji hayo yamempunguzia adha ya kuchota maji kutokana na umri wake mkubwa. Anasema kuna nyakati hasa kiangazi mabwawa yalikuwa yanakauka maji hivyo maisha yanakuwa ya kubahatisha kwani kunakuwa hakuna maji.

Bi. Chuma anasema bei za maji vijijini ziangaliwe ili huduma hiyo iwe endelevu na kuwapa fursa wananachi kufanya kazi zaidi.