Habari

Imewekwa: May, 20 2021

Katibu Mkuu Akutana na Ujumbe wa AfDB Kuhusu Ujenzi wa Bwawa la Farkwa

News Images

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amekutana na wataalam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kufanya mazungumzo kuhusu ujenzi wa bwawa la Farkwa.

Mhandisi Sanga amefanya kikao na wataalam hao katika ofisi za Wizara katika mji wa Serikali Jijini Dodoma.

Wataalam hao wapo katika ziara ya maandalizi ya awali ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Farkwa ambapo Mhandisi Sanga amesema serikali imejiandaa kwa mradi huo ikiwamo kulipa fidia kwa wananchi wanaotakiwa kupisha eneo la ujenzi. .

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeonesha nia ya kushiriki katika kazi ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa.

Akizungumza kwa niaba ya AfDB Bw. Benson Nkhoma amesema awali katika kufanya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huu walifanya vikao viwili mapema mwaka huu kwa njia ya kieletroniki.

Amesema katika vikao hivyo walikubaliana kuwe na ziara ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo kwa kukusanya taarifa na takwimu za msingi.

Watalaam hao kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, pia wamepata fursa ya kufanya kikao na Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango, na Maafisa wa Ofisi ya Makamu wa Rais kujadili kwa upana kuhusu utekelezaji wa mradi wa bwawa la Farkwa linalotarajiwa kuongeza huduma ya maji katika jiji la Dodoma.