Habari

Imewekwa: Sep, 07 2021

Katibu Mkuu Akutana na Ujumbe Kutoka KfW

News Images

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) anayesimamia (Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika) Bw. Christoph Tiskens, makao makuu ya Wizara,Mtumba jijini Dodoma kujadili ushirikiano baina ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Ujerumani katika Sekta ya Maji.

Mhandisi Sanga amefanya mazungumzo hayo na Bw. Christoph aliyeambatana na Dkt. Ralf Wolfgang Orlik anayesimamia Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bw. Christoph Tiskens ambaye ameshika nafasi hiyo katika Ukanda wa Afrika hivi karibuni, alifika Wizarani kujitambulisha. Aidha, majadiliano hayo yamelenga kuongeza ushirikiano zaidi baina ya nchi hizi mbili hususan katika miradi inayoendelea kutekelezwa kupitia ufadhili au usimamizi wa KfW.

Miradi inayotekelezwa kupitia ufadhili wa KfW ni pamoja na Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi (Simiyu Climate Resilience Project), Mradi wa Maji wa Kigoma, Babati na mradi wa maji wa Vwawa Tunduma.

Pamoja na hayo wamezungumzia maandalizi ya majadiliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ujerumani kuhusu awamu zinazofuata za ushirikiano utakao endelezaufadhili wa miradi mbalimbali ya maji.

Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga amemshukuru Bw. Christoph Tiskens kwa kufika ofisi kwake pamoja na Serikali ya Ujerumani kwa ujumla kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) katika kufadhili utekelezaji wa miradi ya maji nchini na sekta hiyo kwa ujumla.

Aidha, Bw. Christoph Tiskens amesema serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza miradi ya maji.

Kitengo cha Mawasiliano