Habari
Jumuiya Zaagizwa Kukabidhi Maeneo Yaliyotangazwa na Serikali Kuwa Maeneo ya Mamlaka za Maji

TAARIFA KWA UMMA
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amezitaka jumuiya, taasisi, vikundi au mtu yeyote anayetoa huduma ya maji katika eneo lililotangazwa na Serikali kuwa eneo la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kutoa huduma ya maji kufanya hivyo mara moja kwa mamlaka husika.
Naibu Waziri Aweso ametoa agizo hilo na kuzitaka Jumuiya ya Watumia Maji Kilema Kusini inayotoa huduma eneo la Njiapanda Mashariki na Kirua Kahe Gravity Water Supply Trust inayotoa huduma eneo la Njiapanda Mgaharibi katika Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro zitimize agizo la Wizara ya Maji kwa kukabidhi maeneo hayo kabla ya tarehe 31 Agosti, 2019.
Na kutoa maelekezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro kupeleka wakaguzi wa hesabu katika taasisi hizo, na ikibainika kuna ubadhirifu wowote wa mali ya umma wahusika wachukuliwe hatua za sheria mara moja.
Maelekezo hayo yametolewa wakati akizindua Mradi wa Maji wa Mwika Kusini uliohusisha uzinduzi wa Chanzo cha Maji cha Kyaronga pamoja na usambazaji wa majisafi wa maeneo ya Kata ya Mwika Kusini katika Wilaya ya Moshi, kazi iliyofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kwa gharama ya Shilingi milioni 726.
Mhe. Aweso ametoa pongezi nyingi kwa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa MUWSA kwa kuendeleza juhudi za kuhakikisha huduma ya majisafi katika mji wa Moshi na maeneo yote inayotoa huduma inaimarika, pamoja matumizi ya rasilimali za mamlaka hiyo katika kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji na usambazaji maji vijijini.
Akawahakikishia wananchi kuwa Wizara ya Maji inaendelea na mchakato wa kuboresha mfumo wa usimamizi wa utoaji wa huduma ya maji katika wilaya za Rombo, Moshi, Hai na Siha na kuwataka viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kusimamia kazi hiyo kwa ufanisi na mafanikio.
Kitengo cha Mawasiliano,
Agosti 20, 2019