Habari

Imewekwa: Mar, 16 2023

​Huduma ya majisafi inatolewa kwa weledi

News Images

Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema mkakati wa kufikisha huduma ya majisafi katika makazi ya wananchi unafanyika kwa weledi kwa kuzingatia maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi.

Mhe. Majaliwa amesema hayo leo tarehe 16 Machi 2023 wakati akifungua rasmi Wiki ya Maji na kuzindua mradi wa majisafi wa Tegeta jijini Dar es salaam. Moja ya maeneo yanayohudumiwa na mradi huo wakazi wake hawajawahi kupata huduma ya majisafi ya bomba katika makazi yao.

Amesema kila kiumbe hai na mazingira vyote vinahitaji maji na wananchi wanapopata huduma ya majisafi, ni maendeleo makubwa katika nchi na kwa mtu binafsi.

“Upatikanaji wa majisafi ni agenda ya kudumu,na inafanyika hatua kwa hatua ili wananchi wapate majisafi ya uhakika kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025 kamaSerikali ilivyopanga” Mhe.Majaliwa amesema na kusisitiza kuwa kazi ya kusambaza maji ni kazi endelevu na kila mwananchi atafikiwa hadi maeneo ya pembezoni.

Amesema Serikali imeanza kutumia vyanzo vikubwa vya maji ili kusambaza maji kwa wananchi, ikiwemo maziwa makuu. Pia, katika kukabilina na mabadiliko ya tabia nchi amesema miradi ya kimkakati inatekelezwa ikiwamo ujenzi wa bwawa la Farkwa na Kidunda, na kuimarisha huduma ya maji katika jiji la Dodoma kwa kutumia bwawa la Mtera.

Mhe. Majaliwa amesema Serikali inao uwezo wa kifedha ambapo vijiji 9,144 vinapata huduma ya maji na lengo ni kufikia vijiji 12,319 na amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji ili huduma ya maji katika makazi yao iwe endelevu na kuitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuhakikisha maeneo yote yanayotoa huduma kwa umma yanapata majisafi.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiongea awali, amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hataki kusikia wananchi wakipata adha ya huduma ya maji na kusisitiza maunganisho ya maji yafanyike ndani ya siku saba za kazi baada ya kupokea maombi.

Mhe. Aweso amefafanua kuwa ni haki ya mwananchi kupata huduma ya maji, ila mwananchi anao wajibu wa kulipia huduma hiyo kadri anavyoitumia.

“Miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita utekelezaji wa bajeti ya Sekta ya Maji umepanda kutoka asilimia 50 hadi asilimia90” Mhe. Aweso amesema na kusisitiza Tanzania inayo maji ya kutosha na watendaji wa Sekta ya Maji wamejipanga kutekeleza miradi ya maji kwa sababu fedha za kazi hiyo zipo.

Mradi wa maji wa Tegeta unanufaisha zaidi ya wakazi laki nne nanusu na umehusisha mfumo wa usambazaji maji kati ya Makongo na mji wa Bagamoyo.

Kitengo cha Mawasiliano