Habari
Dkt. Mpango asisitiza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, amehimiza juhudi za kitaifa katika kuimarisha mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika Kongamano la Nne la Kisayansi la Maji lililoandaliwa na Chuo cha Maji, lenye kaulimbiu "Suluhisho la Maji na Usafi wa Mazingira katikati ya Mabadiliko ya Tabianchi". Mhe. Mpango amesema mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuathiri utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, hususan lengo namba sita linalohusu maji na usafi wa mazingira. Akisisitiza kuwa rasilimali maji ina umuhimu mkubwa sana katika kufikia Malengo ya Maendelo Endelevu, lakini mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa inayoweza kusababisha kutofikiwa kwa lengo hilo.
Mhe. Mpango amekipongeza Chuo cha Maji kwa kuanzisha Jarida la "Journal for Water Engineering Management and Policy" akisisitiza kuwa jarida hilo linapaswa kuwa chombo cha kutoa tafiti zenye manufaa kwa watunga sera na watoa maamuzi
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuboresha miundombinu ya Chuo cha Maji ili kuzalisha wataalam bora wa sekta hiyo.
"Zaidi ya watumishi 9,200 wa Sekta ya Maji nchini wamepitia katika chuo hiki. Ni lazima tuendelee kuwajengea uwezo kupitia mafunzo ya muda mrefu na mfupi, warsha, na makongamano kama haya," Waziri Aweso amesema.
Kongamano hilo linalenga kuendeleza tafiti na miradi bunifu itakayosaidia Sekta ya Maji kuwa na ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na changamoto zote za kisekta. Chuo cha Maji kiazimia kuendelea kuboresha mitaala yake na kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Maji ili kuhakikisha ufanisi wa sekta hiyo nchini Tanzania.