Habari
Kazi ya Kusambaza Miundombinu ya Maji Mradi wa Same-Mwanga-Korogwe yaendelea Vizuri

Siku moja baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa Maji wa Same -Mwanga- Korogwe Septemba 24, 2021, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Wizara hiyo Joyce Msiru eneo linakofanyika kazi ya usambazaji wa mabomba inayofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Mhandishi Kemikimba ameridhishwa na hatua iliyofikiwa baada ya kukagua kazi hiyo na kuwataka DAWASA wakamilishe kazi hiyo kwa wakati ili huduma ya maji ianze kupatikana kwenye baadhi ya maeneo kabla ya mradmradi sote kukamilika kwa asilimia 100.
"Baada ya kutembelea maeneo yote, nimeridhika na jitihada zinazofanywa na DAWASA, nafahamu kuwa moja ya agizo la Waziri Mkuu ni kuhakikisha vijiji ambavyo tulikuwa hatujaanza utekelezaji vikiwemo vinavyozunguka eneo la chanzo cha maji tunavifikia ili maji yakianza kutoka, na wao wapate huduma. Nawahakikishia wananchi kuwa kazi hiyo tutaifanya kwa haraka bila kuchelewa." Mhandisi Kemikimba amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi DAWASA Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema utekelezaji wa mradi huo unakwenda vizuri na kumhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa kazi hiyo itakamilika ndani ya wakati.
"Katika eneo la Mwanga tulitakiwa kusambaza mabomba kilometa 53, tumeshasambaza Kilometa 49. Upande wa Same tumesambaza kilometa 3 kati ya 15. Lengo ni kukamilisha kilometa zilizobaki mwishoni mwa mwezi Oktoba 2021." Mhandisi Mtindasi amesema.
Mradi wa Same - Mwanga-Korogwe unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 262 na unatarajia kuhudumia wananchi zaidi ya 400,000.