Habari
Bilioni 8.26 kutatua tatizo la maji Bukene Nzega

Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 8.26 kufikisha majisafi na salama kwa wananchi wa Kata ya Bukene, wilayani Nzega katika mkoa wa Tabora kwa kutumia maji ya mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Viktoria umbali wa kilomita 34 ili kutatua changamoto kubwa ya maji inayoikabili kata hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) alipokuwa akikagua miradi ya maji katika Kata ya Bukene na kuwaahidi wakazi wa Bukene kunufaika na mradi wa maji wa Igunga-Nzega-Tabora unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni wa mwezi Novemba, 2019.
Mradi wa maji wa Igunga-Nzega-Tabora umegharimu shilingi bilioni 604, na kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 85 utakapokamilika utanufaisha wakazi wapatao milioni 1.2.
Aidha, serikali imejipanga pia kutatua tatizo la maji katika Kata ya Nkinga, Wilaya ya Igunga ambapo itajenga mtandao wa maji kwa kutandika bomba kutoka bomba kuu lenye urefu wa takribani kilomita 25 na kujenga tenki la juu la mita 12 litakalosambaza maji kwa wananchi.
Akiwa wilayani Nzega, Prof. Mbarawa ameelekeza pampu moja kati ya mbili zilizopo katika wilaya hiyo ipelekwe Wilaya ya Sikonge ikatumike ili kurejesha huduma ya maji, kutokana na pampu yao kuungua wakati utaratibu wa kununua pampu mpya ukiendelea.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa ameelekeza Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo kufanya uchunguzi kwa Kamati ya Watumia Maji Nkinga na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya ubadhilifu wa fedha za makusanyo ya maji za mradi huo.
Kitengo cha Mawasiliano