Habari

Imewekwa: Jul, 12 2019

Bilioni 3.2 Kutumika Kumaliza Tatizo la Maji Kibondo

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la maji katika mji wa Kibondo kwa kutumia Shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mabamba-Mkarazi utakaotoa huduma ya maji ya uhakika na kutosheleza kwa wananchi katika vijiji vya Mabamba, Mkarazi na Kitahana vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kitahana, Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema fedha hizo zimetolewa ili kutimiza ahadi ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli ya kuwapatia wakazi wa Kibondo huduma ya maji, wakati akikagua hatua za utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Mabamba-Mkarazi katika Wilaya ya Kibondo.

‘‘Kibondo ni miongoni mwa miji yenye uhaba wa maji, kwa kutambua hilo tumetoa bilioni 1.2 kwa Mradi wa Maji wa Mabamba-Mkarazi na tutatoa bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi wa mradi mwingine wa maji kwa wakazi wa Kibondo’’, Naibu Waziri Aweso ameahidi.

‘‘Dhamira ya Rais Magufuli ni kumtua Mama Ndoo Kichwani na kama wizara tunatekeleza maagizo hayo na nimejionea mradi umeanza kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi, kazi iliyobaki ni mkandarasi kumalizia ujenzi wa vilula vilivyobaki”, Naibu Waziri Aweso ameelekeza.

Mradi wa Maji wa Mabamba-Mkarazi umefikia asilimia 70 ya ujenzi wake chini ya Mkandarasi; Kampuni ya KKG Investment (T) Ltd iliyochukua kazi hiyo kutoka kwa Kampuni ya Motomoto iliyositishiwa kazi na Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) baada ya kutoridhishwa na kasi ya utendaji wake.

Awali, Naibu Waziri Aweso ametoa matumaini kwa wakazi wa mji wa Mwandiga uliopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kuwa ifikapo mwezi Agosti, itatoa kiasi cha Shilingi milioni 500 za kuanzia kazi ya ujenzi wa miundombinu itakayopeleka huduma ya maji kwa wananchi kutoka kwenye Mradi wa Maji wa Kigoma Mjini.

Kitengo cha Mawasiliano

12 Julai, 2019