Habari

Imewekwa: Dec, 02 2025

Aweso Acha Neema Kivule, Azindua Utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Sh. Bilioni 2.7

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), ameacha neema kwa wakazi wa Kivule baada ya kuzindua rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Kivule wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 2.7.

Katika ziara yake ya kikazi iliyofanyika Kata ya Majohe, wilayani Ilala, Jijini Dar es Salaam, Waziri Aweso alikabidhi mabomba ya ukubwa mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, huku akishuhudiwa na Mbunge wa Jimbo la Kivule, Mhe. Ojambi Massaburi.

Amesema mradi huu, unaotekelezwa kwa fedha za bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, ni mojawapo ya hatua muhimu za Serikali katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

“Tunatambua changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Kivule. Kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), tunaanza kutekeleza mradi mkubwa wa Sh. bilioni 2.7 ili kutatua tatizo hilo,” amesema Waziri Aweso.

Aidha, ametoa maelekezo kwa Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) kupeleka magari mawili maalumu kwa ajili ya kuchimba visima, hatua itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Kivule.

“Nataka magari haya yafike haraka na visima vyenyewe vichimbwe ili kuhakikisha wakazi wanapata maji ya kutosha,” amesema Waziri Aweso.

Akiwa Kata ya Majohe, Waziri Aweso alikabidhiwa mapokezi ya shangwe na mamia ya wakazi wa Kivule, wakiongozwa na Mbunge wa eneo hilo, Mhe. Ojambi Massaburi. Mbunge na wakazi walieleza matumaini yao makubwa kwa Serikali na kushukuru hatua zilizochukuliwa za kutatua kero zao za maji.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amethibitisha kuwa fedha za mradi zitahakikishiwa zinapatikana na kufika kwa wakati ili utekelezaji wake ukamilike bila ucheleweshaji.