Habari
Aweso Akemea Ubadhirifu wa Fedha za Jumuiya ya Watumia Maji – Berege Mpwapwa

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amekemea vikali ubadhirifu wa fedha za Jumuiya ya watumia maji katika mradi wa maji wa Berege Wilayani Mpwapwa katika Jiji la Dodoma.
Waziri ametoa kauli hiyo ya kukemea wakati alipofanya ziara ya kikazi kukagua utekelezaji na uendeshaji wa miradi ya maji pamoja na kuzungumza na wananchi katika kijiji cha Berege kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
“Nimebaini fedha za Jumuiya ya Watumia Maji hapa Berege zinaliwa na hakuna usimamizi mzuri wala utunzaji mzuri wa taarifa za fedha, hivyo nakuagiza Mkuu wa Wilaya ufanyike ukaguzi maalum (special audit) katika akaunti ya Jumuiya hii ili kuweza kubaini fedha zote zilizoliwa na hatua kali zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na ubadhilifu wa fedha katika mradi huu” Waziri Aweso amesema.
Amesema Jumuiya za Watumia Maji nchini zimekuwa zinaajiri watu wasiokuwa na sifa, hivyo amesisitiza kuwa kuanzia sasa Jumuiya zote za watumia maji nchini ziajiri mafundi sanifu wanaomaliza kutoka Chuo cha Maji na kuajiri Wahasibu wenye sifa ya Uhasibu.
“Jumuiya nyingi za maji zimekuwa zikivunjika kutokana na changamoto za watu kuingia na kujichukulia pamoja na kula pesa za uendeshaji wa miradi ya maji, niwahakikishie wananchi wote waliokula fedha za mradi huu na maeneo mengine nchini wajue watazitapika,” Waziri Aweso amesisitiza.
“Natuma salamu kwa Jumuiya za Watumia Maji nchini kuacha tabia ya kuajiri watu wasiokuwa na sifa na badala yake waajiri wahasibu na Mafundi Sanifu wenye sifa na kuhakikisha taarifa za mapato na matumizi ya fedha zinatolewa kila wakati,” Waziri Aweso amesema.
Aidha, amemuagiza Meneja wa RUWASA Mpwapwa, Mhandisi Syprian Warioba kurejesha fedha zilizochukuliwa katika Jumuiya ya Watumia Maji Berege kuwalipa wataalam kwa ajili ya usimamizi wa miradi kwa kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amemuagiza Meneja wa Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA) Peter Mdalangwila kuhakikisha wanafika Mpwapwa ifikapo Jumamosi tarehe 29 Mei, 2021 kuchimba visima vitatu katika Wilaya hiyo na kati ya visima hivyo kimoja kichimbwe katika Shule ya Sekondari Mpwapwa ili kupunguza adha ya maji inayowakabili wanafunzi shuleni hapo.
Kitengo cha Mawasiliano