Habari
Teknolojia ya Amanzi Yapongezwa na Wizara ya Maji

Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Wizara ya Maji, Joash Nyitambe, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) kwa hatua kubwa ya kutumia mfumo wa kidigitali wa kuripoti mivujo ujulikanao kama Amanzi (Amanzi App). Mfumo huu umetajwa kuwa chachu ya mageuzi katika Sekta ya Maji, ukisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza na kudhibiti upotevu wa maji.
Akizungumza katika ziara yake ya kikazi mjini Kigoma, Nyitambe amesema kuwa hatua ya KUWASA kutumia teknolojia katika kusimamia huduma za maji ni mfano bora wa kuigwa na mamlaka nyingine kote nchini.
“Tunajivunia kuona teknolojia ikitumika kuboresha huduma na kutatua changamoto za wananchi. Hongereni sana kwa hatua kubwa hii ya kiubunifu ambayo inagusa moja kwa moja maisha ya wananchi,” Nyitambe amesema.
Katika ziara hiyo, Nyitambe alipata fursa ya kutembelea maeneo kadhaa na kujionea namna mfumo wa Amanzi unavyofanya kazi kwa ufanisi. Alisisitiza kwamba matumizi ya teknolojia bora kama huu si tu yanarahisisha huduma, bali pia yanathibitisha kuwa sekta ya maji inaweza kuwa kinara katika uvumbuzi na matumizi ya TEHAMA kwa manufaa ya jamii.
Amanzi ni mfumo maalum wa kuripoti mivujo uliobuniwa na Kampuni ya Collect Tech. Mfumo huu unafanya kazi kwa namna , ambapo mwananchi anapobaini mvujo katika eneo lolote, anaweza kutoa taarifa papo hapo kupitia simu yake ya mkononi.
Baada ya taarifa hiyo kupokelewa na mfumo, mafundi wa KUWASA hukimbilia eneo husika kwa haraka na kuchukua hatua za kudhibiti mvujo huo. Utaratibu huu umeleta mapinduzi makubwa kwa kuokoa maji yaliyokuwa yanapotea bila sababu, na hivyo kuongeza ufanisi wa usambazaji maji kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Nyitambe, mfumo huu ni ushahidi tosha kwamba matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kuleta mabadiliko chanya, kuongeza uwajibikaji, na kuhakikisha huduma za maji zinatolewa kwa ubora wa hali ya juu. Aliitaka KUWASA kuendelea kusimamia vizuri mfumo huu na akazitaka mamlaka nyingine nchini kuiga mfano huo kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Mfumo huu umeundwa si kwa ajili ya KUWASA pekee, bali pia kwa kushirikisha wananchi moja kwa moja katika kulinda rasilimali ya maji. Kupitia Mfumo wa Amanzi, kila mmoja ana nafasi ya kushiriki katika kutunza rasimali maji.