Habari
Waziri Aweso na RC Makalla wakubaliana Kuimarisha Ushirikiano Katika Usimamizi wa Sekta ya Maji Mkoani Arusha
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amosl Makalla kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi na utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo.
Katika mazungumzo hayo, RC Makalla ameelezea dhamira ya Mkoa wa Arusha kudhibiti wizi wa dira za maji unaoripotiwa katika baadhi ya maeneo.
Aidha, amempongeza Waziri Aweso kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimhakikishia ushirikiano mkubwa katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo.
"Ni wazi kuwa uhodari wako, ubunifu na uchapakazi wako vimemshawishi Mheshimiwa Rais kuendelea kukuamini. Sisi tuliopo mikoani tunashuhudia kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Maji hapa Arusha na hata maeneo mengine nchini, katika kuboresha huduma za maji mijini na vijijini. Ninaridhishwa sana na namna tunavyoshirikiana," RC Makalla amesema.
Kwa upande wake, Waziri Aweso amemshukuru RC Makalla kwa upendo na ushirikiano wake, akimpongeza kwa usimamizi wake wa karibu kwenye Sekta ya Maji.
Akimhakikishia kuwa ataendeleza na kusimamia kikamilifu misingi aliyoiweka alipokuwa Naibu Waziri wa Maji, hususan katika mapambano dhidi ya wizi na upotevu wa maji yaliyokuwa yakikabili sekta hiyo katika kipindi chake cha uongozi.

