Habari

Imewekwa: Feb, 04 2024

Wizara ya Maji yapewa kongole kwa ushirikishaji wananchi miradi ya maji

News Images

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imepongeza watendaji wa Wizara ya Maji kwa ushirikishaji mzuri wa wananchi wakati wa kutekekeza miradi ya maji.

Pongezi hizo zimetolewa baada ya Kamati hiyo kutembelea Mradi wa Maji wa Miji 28 katika miji ya Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui ambapo ulazaji wa mabomba unaendelea kwa umbali wa kilometa 111.22 kuelekea katika viunga vya miji hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) amesema ushirikishwaji ndio njia nzuri ya kuondoa malalamiko na kuwezesha miradi kukamilika kwa haraka na kwa wakati.

Awali akiwasilisha taarifa ya Mradi mratibu wa Mradi huo Mhandisi Edward Tindwa amesema changamoto wanayokutana nayo kwa sasa ni kilimo ambacho kinaendelea katika maeneo unakopitia mradi lakini mara zote wamewashirikisha wananchi na wanatoa ushirikiano na kuruhusu mabomba ya maji kupita.

Aidha, Kamati hiyo imeendelea kusisitiza utunzaji wa miundombinu ya maji na kuhakikisha maji yanayozalishwa na miradi hiyo inasambazwa kwa wananchi.

Pamoja na hayo kamati hiyo imetembelea Mradi wa Ukarabati wa Bwawa la Igombe na kuridhishwa na utekekezaji wake.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) alimwakilisha Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb).

Mhe. Mahundi amesema Wizara ya Maji inaendelea na jitihada ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote. Amesema kukamilika kwa mradi wa Maji wa Miji 28 mkoani hapo kutawezesha huduma ya maji kutoka ziwa Victoria kuzifikia wilaya zote za mkoa wa Tabora.

Amesema wataendelea kusimamia ili kuhakikisha watanzania wote wananufaika na huduma ya majisafi na salama.


Bwawa la maji la Igombe limekarabatiwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7 na limekamilika kwa asilimia mia moja wakati Mradi wa Maji wa Miji 28 unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 143.26 na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2025.