Habari

Imewekwa: Sep, 18 2021

​Waziri Mkuu awataka RUWASA Kukamilisha Mradi wa Maji wa Kifura Haraka

News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amemtaka Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Mathias Mwenda kuhakikisha mradi wa maji wa Kifura, wilayani Kibondo unakamilika ifikapo Februari 2022.

Mhe. Majaliwa ametoa agizo hilo Septemba 17, 2021 alipotembelea na kukagua mradi huo ambao unatarajia kuwanufaisha wananchi wapatao zaidi ya elfu 12 wa kijiji cha Kifura.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya majisafi na salama, hivyo watendaji wa Serikali wanapaswa kusimamia hilo kwa ukaribu.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amedhamiria kupeleka maji kwa kila Mtanzania. Anafahamu jinsi akinamama, vijana na Watanzania wote wanavyohangaika kutembea kwa miguu, bodaboda na baiskeli wakiwa na madumu ya maji. Kwa hiyo anafanya kila njia kuhakikisha huduma hii inamfikia kila Mtanzania” Mhe. Majaliwa amesema.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Kigoma Mhandisi Mathius Mwenda amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi kampuni ya M/S NANGAI Engineering and Contractors Co. Ltd kwa Gharama ya Euro 880,256.54 sawa na shilingi bilioni 2,405,741,123.83 za Tanzania.

Amesema fedha hiyo ya utekelezaji wa mradi ipo, hivyo mradi huo utakamilika kwa wakati.

Amewataka wananchi wanaohitaji kuunganishiwa maji majumbani wajitokeze. Aidha, amesema mradi huo una vituo vya kuchotea maji vya Umma vipatavyo 50 ambavyo vitasaidia kuondoa kabisa changamoto ya Maji katika kijiji hicho.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amempongeza Rais Samia kwa kuimarisha mahusiano na nchi za nje. Amesema mahusiano hayo mema ndio yamewezesha Serikali ya Ubelgiji kusaidia utekelezaji wa mradi huo. Amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati.

Mradi wa maji Kifura ni moja ya miradi ambayo inatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ubelgiji mkoani Kigoma.