Habari

Imewekwa: Feb, 25 2026

​Waziri Mkuu Aagiza Maeneo ya Huduma kwa Umma Yapate Huduma ya Majisafi na Salama

News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mwigulu Nchemba (Mb) amepongeza hatua iliyofikiwa katika utoaji wa huduma ya maji nchini na kuagiza nguvu ielekezwe kuhakikisha maeneo yanayotoa huduma kwa umma ikiwamo shule, na vituo vya huduma za afya huduma ya majisafi na salama ya uhakika inakuwepo.

Ametoa agizo hilo akifungua mkutano wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ngurdoto, mkoani Arusha.

Amesema Wizara ya Maji imeweza kutafsiri kwa usahihi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Mama wa Kitanzania 'anatuliwa ndoo ya maji kichwani'.

Hata hivyo, amesisitiza kazi iendelee ili kuhakikisha ufumbuzi unapatikana katika maeneo ambayo bado hayajapata huduma.

Aidha, amewataka wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji kutumia fursa ya mafunzo wanayoyapata kutatua changamoto za maeneo yao na akasisitiza mikakati ya kuzuia upotevu wa maji na wizi wa maji.

Vilevile, ametoa rai kuhusu kutunza miundombinu ya maji pamoja na vyanzo vya maji ni jukumu la wananchi wote na sio Serikali pekee.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amezindua rasmi Mfumo wa Maunganisho ya Huduma ya Maji Kidijitali pamoja na Mkakati wa Ufungaji wa Dira za Maji za Malipo ya Kabla (Pre-paid meters) kwa dhumuni la kuimarisha huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema uwekezaji mkubwa utafanyika kwenye teknolojia kwa dhumuni kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.

Amebainisha kuwa kipaumbele cha Wizara ya Maji ni kuboresha eneo la huduma kwa mteja.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amesema Wizara ya Maji imejipanga kutimiza lengo la kufikisha huduma kwa wananchi kwa asilimia mia moja.

Wizara ya Maji inaendesha mafunzo kwa wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira lengo likiwa kuwawezesha Wajumbe wa Bodi hizo kutekeleza majukumu yao kwa ufanikishi ili kuharakisha jitihada za kufikisha huduma ya maji kwa kila Mtanzania ifikapo mwaka 2030.