Habari
Maji Kuwafikia Wananchi kwa Asilimia 100

Serikali inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za maji safi na salama ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa asilimia 100.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Mb) amesema wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi ya ziwa Victoria kutoka eneo la Makomero - Mgongoro, kijiji cha Mwamayoka, Igunga mkoani Tabora.
Thamani ya mradi huo ni shilingi milioni 840.8 na unanufaisha zaidi ya wakazi elfu tano.
“Ndugu zangu mradi huu ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuweni na uhakika kwamba Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayewajali, anawapenda na anasikiliza changamoto zenu, endeleeni kutekeleza majukumu yenu ipasavyo kwasababu tunaye kiongozi madhubiti” Majaliwa
Ameiagiza Wakala ya Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA kusogeza vituo vya umma vya kuchota maji karibu na wananchi.
Mradi umefika asilimia 80 ya ujenzi na unahusisha ujenzi wa vituo sita vya umma kuchota maji, ukarabati wa vituo sita vya umma kuchota maji, ukarabati wa mabirika mawili ya maji kwa ajili ya mifugo, kuchimba mitaro ya kulaza bomba na kufukia mitaro mita 25,000.