Habari
Miradi ya Maji Yaendelea Kutekelezwa Nchini-Waziri Mkuu

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya majisafi na salama katika maeneo yao ya makazi.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema hayo akiwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza, alipokuwa akizungumza na wananchi wa eneo la Hungumalwa mara baada ya kuzindua rasmi Mradi wa Maji Hungumalwa. Amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama Tawala.
“Tutaendelea kusimamia maelekezo ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na tutaendelea kutekeleza ilani kwa vitendo. Tutawahudumia wananchi wala msiwe na mashaka. Suala la maji tunaendelea kuhakikisha yanapatikana maeneo yote,” Waziri Mkuu Majaliwa amesema.
Ameongeza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote, na hivyo kuwaomba waendelee kuiamini na kushirikiana na Serikali yao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Godfrey Sanga, amesema mradi huo umegharimu jumla ya shilingi bilioni 11. Kati ya kiasi hicho, kazi zilizokamilika hadi sasa zina thamani ya shilingi bilioni 10, na hivyo kubakia salio la shilingi milioni 201 katika mkataba wa ujenzi.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umehusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita milioni moja, ulazaji wa mabomba na viungio vyake yenye urefu wa kilomita 54.817, uchimbaji na ufukiaji wa mitaro yenye urefu huo huo, pamoja na kuunganishia huduma ya maji kwa wateja wa majumbani wapatao 500.
Aidha, umejengwa pia ofisi ya Chombo cha Watumia Maji ngazi ya jamii pamoja na nyumba ya mlinzi, ambapo kazi zote zimekamilika kwa mafanikio.
Mradi wa Maji Hungumalwa ulianza kutekelezwa tarehe 8 Machi 2022 na umekamilika rasmi tarehe 15 Agosti 2024.