Habari

Imewekwa: May, 21 2025

Kamati ya Bunge ya Bajeti Yapokea Taarifa ya Utekelezaji wa Mfuko wa Taifa wa Maji

News Images

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imepokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Taifa wa Maji kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo, Wakili Haji Nandule, katika kikao rasmi kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Naibu Waziri wa Maji, Wakili Nandule alieleza kuwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Maji kulilenga kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha za uhakika kwa ajili ya kuchochea kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini. Alibainisha kuwa miradi hiyo inalenga kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi, salama na ya kutosheleza kwa wananchi, sambamba na kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji kwa misingi ya maendeleo endelevu.

Katika utekelezaji wake, Mfuko wa Taifa wa Maji umeendelea kuwa muhimili wa utekelezaji wa miradi kwa kutoa miongozo ya kisera na kiutekelezaji kuhusu utoaji wa fedha, pamoja na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinasimamiwa kikamilifu kupitia mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini. Taarifa iliyowasilishwa imeonesha namna Mfuko unavyosimamia uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali fedha kwa ajili ya kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

Wakili Nandule pia ameeleza kuwa Mfuko wa Taifa wa Maji umeendelea kuimarisha juhudi za kuongeza mapato ya ndani kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kisera na kimkakati ya kuhakikisha uendelevu wa rasilimali hizo. Miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na kujenga hoja ya msingi kwa Serikali ili kuongezewa mgao kutoka katika tozo ya mafuta ya petroli na dizeli, jambo litakaloongeza uwezo wa kifedha wa Mfuko na kuwezesha uboreshaji mkubwa wa miradi ya maji vijijini na mijini.

Aidha, taarifa hiyo imeweka bayana mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, changamoto zilizopo, na mapendekezo ya kimkakati kwa ajili ya kuendelea kuimarisha utendaji wa Mfuko na mchango wake katika kufanikisha ajenda ya Taifa ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji, kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya Taifa na malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).