Habari
Hatimaye Maji ya Ziwa Victoria Yafika Sikonge
Historia imeandikwa mara baada ya maji kutoka Ziwa Victoria kufika rasmi katika Mji wa Sikonge, tukio lililoshuhudiwa na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28, mkoani Tabora.
Akizungumza baada ya kushuhudia tone la kwanza la maji, Waziri Aweso amesema jukumu lake kama Waziri wa Maji ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama, huduma ambayo huleta tabasamu na kuboresha maisha yao.
“Rais Samia ametuelekeza Mawaziri wote kuhakikisha kazi yetu inaleta tabasamu kwa wananchi, na mimi ninatimiza wajibu wangu kwenu,” Aweso amesema. Ameongeza kuwa hatua inayofuata ni kukamilisha kazi ya ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji ili huduma hiyo iwafikie wananchi moja kwa moja.
Kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28, unaoendeleza utekelezaji wa Mkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji ambapo vyanzo vikubwa vya maji nchini vinanufaisha maeneo yenye uhaba wa maji, miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua iinatarajiwa kunufaika na maji yanayotoka Ziwa Victoria.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso ameelekeza Shilingi milioni 500 zitolewe mara moja kwa ajili ya kuanza kazi ya usambazaji wa maji kwa wananchi kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Urambo, mkoani Tabora.
Ametoa maelekezo hayo baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, ambapo ametoa muda wa wiki tatu kukamilisha kazi zilizobaki, ikiwemo ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa mita 650 hadi kwenye tenki la kuhifadhi maji pamoja na kufanya majaribio ya tenki hilo.
Aweso amesisitiza kuwa kazi zote zilizobaki ni lazima zikamilike ifikapo mwisho wa mwezi Februari, 2026, na kwamba ukamilishaji wa kazi hizo uendane sanjari na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji kwa wakazi wa Urambo ili waanze kunufaika na huduma hiyo.
Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, inaendelea kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji nchini kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28 unaojumuisha miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua mkoani Tabora, ukitumia Ziwa Victoria kama chanzo kikuu cha maji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 11 Aprili, 2023, na unatarajiwa kukamilika tarehe 10 Julai, 2026.
Ameeleza kuwa mradi unatekelezwa na Mkandarasi Megha Engineering and Infrastructure Ltd chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri WAPCOS Ltd, kwa gharama ya takribani Shilingi bilioni 143.26. Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2026, utekelezaji wake umefikia asilimia 76.
Mradi utakapokamilika, unatarajiwa kuzalisha lita 24,760,000 za maji kwa siku, ikilinganishwa na uzalishaji wa sasa wa lita 271,300 pekee kwa siku, na kuhudumia zaidi ya wakazi 490,926 wa Wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui pamoja na vijiji 63.
Kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Sikonge kunaweka alama muhimu kwa Mkoa wa Tabora, ambapo wilaya zake zote saba (7) zitakuwa zimepata maji kutoka Ziwa Victoria, hatua inayothibitisha jitihada kubwa za Serikali katika kumkomboa mwananchi dhidi ya adha ya maji na kumtua mama ndoo kichwani.

