Habari
Watendaji Wizara ya Maji Watakiwa kusambaza maji Mradi wa maji Mugango Kiabakari Butiama

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amekagua mradi wa maji wa Mugango Kiabakari Butiama na kuagiza watendaji wa Wizara ya Maji kuhakikisha wanaongeza nguvu katika usambazaji maji kwa wananchi.
Amesema mradi huo umetekelezwa na kukamilika, kazi iliyopo ni kuhakikisha maji hayo yanasambazwa kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Amesema wananchi wanaonufaika na huduma ya maji katika mradi huo ni kwa sasa ni takribani 2900, maji yanayozalishwa ni lita milioni 17 kwa siku ambazo zinaweza kutosheleza watu wengi zaidi kwa hivyo watendaji wa Wizara ya Maji wanapaswa kufanya kazi zaidi kuifikia jamii.
Amesisitiza kuwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kila mwananchi anafikishiwa huduma ya majisafi na salama, pia kuwa na Gridi ya Taifa ya Maji ambapo mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kufanikisha hilo.
Pamoja na mradi huo ambao chanzo chake ni ziwa Victoria, ipo miradi mingine mkoani hapo ambayo inaendelea kutekelezwa kwa kutumia vyanzo vya uhakika vya maji. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji wa Rorya Tarime ambao utafika hadi Sirari, pia mradi wa wa miji 28 katika mji wa Mugumu
“Miradi yote hii inatumia vyanzo vya uhakika vya maji hivyo niwahakikishie Watanzania kwamba malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itafikiwa na kuondoa kabisa changamoto ya huduma ya majisafi na salama kwa kila mwananchi.
Katika ziara hiyo Mhandisi Mwajuma ameambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Maji wa Taifa Mhandisi Abdallah Mkufunzi ambaye ameahidi kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya usambazaji wa maji katika mradi huo.