Habari
Wahandisi watakiwa Kusimamia Miradi ya Maji kwa Ukaribu

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amewataka wahandisi wa maji nchini kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji kwa ukaribu, kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ubora ili kufikia lengo la kufikisha huduma ya maji kwa maeneo yote mijini na vijijini.
Mhe. Waziri Mkuu amesema hayo katika Kikao cha Watendaji wa Sekta ya Maji kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma akisema kuwa changamoto kubwa kwenye Sekta ya Maji ni ucheleweshaji wa miradi, inayochukua muda mrefu kukamilika na kukwamisha azma ya Serikali ya kuleta maendeleo nchini.
Akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejizatiti kuleta mageuzi kwenye Sekta ya Maji kwa lengo la kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025.
Aidha, Mhe. Waziri Mkuu amezindua rasmi Mwongozo wa Usanifu wa Miradi ya Maji (Design Manual) utakaotumika kwenye ujenzi wa miradi yote ya maji nchini, pamoja na kugawa pikipiki 147 zilizotolewa na Serikali kwa Wakala wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa miradi ya maji kwenye halmashauri zote nchini na magari matatu (3) ya majitaka kwa Mamlaka za Maji.
Awali, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema wizara itahakikisha fedha zote za utekelezaji wa miradi ya maji zinasimamiwa na kutumika ipasavyo na hatamvumilia mkandarasi wala wataalam yoyote atakayeonekana kukwamisha juhudi za Serikali za kufikisha huduma ya majisafi, salama na ya kutosheleza kwa wananchi.