Habari
Wafanyakazi Maji Watakiwa Kuzingatia Utendaji Wenye Matokeo

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amewataka watumishi wa Wizara ya Maji kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, na miongozo mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.
Amesema hayo wakati akifungua kikao cha Baraza Dogo la Wafanyakazi wa Wizara ya Maji Makao Makuu, jijini Dodoma.
Mhandisi Kemikimba amesema ni wajibu wa kila mfanyakazi wa Wizara ya Maji kuhakikisha anafahamu wajibu wake mahala pa kazi, anatekeleza malengo aliyopangiwa kwa muda sahihi kwa kufanikisha lengo kuu la Wizara la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama.
“Baraza hili lina wajibu mkubwa wa kusimamia, kushauri na kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao, pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo bora ya utendaji wa kazi yenye tija, staha na upendo”, Naibu Katibu Mkuu Kemikimba amesema.
“Uongozi wa Wizara ya Maji umelenga kuifanya wizara kuwa kitovu cha utendaji bora chenye kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ili kuendana na wakati kwa kuweka mipango na mikakati madhubuti itakayofanikisha utekelezaji wenye matokeo ya haraka, uhakika na endelevu”, Mhandisi Kemikimba amefafanua.
Pamoja na hilo, Mhandisi Kemikimba amewasisitiza wafanyakazi wa Wizara ya Maji kuendeleza jitihada za kujikinga na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UVIKO19 nchini kwa kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalam wa afya, ikiwa ni pamoja na kupata chanjo kwa hiari kwa kuwa mtaji mkubwa wa Serikali ni Rasilimali watu wenye afya bora.
Awali, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maji, Samwel Mhadisa amesisitiza kuwa ni jukumu la kila mfanyakazi kujua wajibu wake na kutumia muda wake wa kazi ipasavyo kwa bidii, juhudi na maarifa ili kufanikisha malengo ya wizara kwa wakati na mafanikio makubwa.
Baraza la Wafanyakazi limeundwa kwa kuzingatia Agizo la Rais la Mwaka 1970 na miongozo mingine. Lengo ni kuitekeleza sera ya ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi na utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa pamoja katika sehemu za kazi.