Habari
Bilioni 81 Kumaliza Changamoto ya Maji Morogoro
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Mtambo wa Kutibu Maji kutawezesha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) kuongeza uzalishaji wa maji kwa lita milioni 54 kwa siku, kutoka uwezo wa sasa wa kuzalisha lita milioni 47 kwa siku. Hatua hiyo itaifanya jumla ya uzalishaji wa maji kufikia lita milioni 101 kwa siku, ikilinganishwa na mahitaji ya sasa ya lita milioni 81.25 kwa siku, hali itakayotosheleza mahitaji ya maji ya Mji wa Morogoro kwa asilimia 100.
Waziri Aweso ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa Uenzi wa Mtambo mpya wa Kutibu Maji-Mafiga wenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni 81.41 ambao utazalisha lita Milioni 54 kwa siku ili kuboresha Huduma ya Majisafi katika Manispaa ya Morogoro.
Mradi huu, unaogharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ni sehemu ya Mradi mkubwa wa Kuboresha Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira wenye thamani ya takribani Sh. bilioni 200 ukiwa chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morgoro (MORUWASA).
Akizungumza katika hafla hiyo Aweso amesema Serikali imedhamiria kumaliza kilio cha muda mrefu juu ya adha ya upatikanaji wa maji kwa kuhakikisha inatekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji katika Bwawa la Mindu kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro.
Waziri Aweso ameitaka MORUWASA kuhakikisha wanatumia utaalamu na uweledi wote walio nao kumsimamia Mkandarasi kutekeleza kazi hii katika ubora unaolingana na thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati kama ulivyopangwa ili Wananchi wanufaike na uwekekezaji huo.
Aidha, Aweso ameahidi ushirikiano wa karibu na wadau wote wa Sekta ya Maji kwa dhumuni la kuendeleza kasi ya utendaji ili kuhakikisha mipango ya Serikali ya kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Watanzania wote mijini na vijijini inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango ili wananchi waweze kufikiwa na huduma iliyo bora ya majisafi na salama na yenye kutosheleza.
Pia, amewasihi wananchi wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kutunza vyanzo hivi vya maji, hususani wananchi wanaoishi milimani ambapo vyanzo vingi vimeanzia huko. Uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji unasababisha janga la ukame, suala ambalo hatimaye husababisha ukosefu wa maji kwa matumizi ya binadamu na kwa shughuli za maendeleo zikiwemo kilimo, viwanda, uvuvi na ufugaji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ili kuhakikisha ukukuaji wa miji unaenda sanjari na upatikanaji wa huduma ya maji.
Amesema mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation kwa kushirikiana na Shanghai Municipal Engineering Design Institute (Group) Co. Ltd, ambapo kukamilika kwake kutanufaisha wananchi zaidi ya 602,000 wa Manispaa ya Morogoro na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 24 kwa lengo la kutoa huduma ya majisafi na salama kwa matumizi ya majumbani, viwandani na shughuli nyingine za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Celine Robert ameelezea manufaa makubwa ya ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na AFD katika mikoa ya Morogoro, Mwanza, Shinyanga na Mara ambapo imetoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Sekta ya Maji.

