Habari
Tanzania na Ujerumani Kuendeleza Uhifadhi wa Maeneo Oevu ya Katuma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji, kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), zimesaini mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Uhifadhi wa Maeneo Oevu na Bioanuwai katika Kidakio cha Katuma, unaofahamika kama Mradi wa IKI Katuma.
Mradi huu wa kimkakati utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na utagharimu kiasi cha Euro milioni 4.0, sawa na takriban shilingi bilioni 11 za Kitanzania, zikiwa ni msaada kutoka Serikali ya Ujerumani kupitia Mfuko wa Kimataifa wa Hali ya Hewa (IKI – International Climate Initiative).
IKI Katuma unalenga kuzijengea uwezo taasisi mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa rasilimali za maji kwa njia shirikishi, huku ukijikita katika kuimarisha mshikamano kati ya sekta mbalimbali kama maji, mazingira, ardhi, misitu na jamii za pembezoni mwa maeneo oevu ya Katuma. Mradi huu unakusudia kuimarisha huduma za mifumo ya ikolojia, ikiwemo uhifadhi wa vyanzo vya maji, udhibiti wa mafuriko, uhifadhi wa bioanuwai, na kuendeleza maisha ya jamii zinazotegemea mfumo huu wa asili.
Kupitia utekelezaji wa mradi huu, taasisi za serikali na wadau wa maendeleo watawezeshwa katika kupanga na kusimamia matumizi bora ya ardhi kwenye eneo la kidakio, pamoja na kuimarisha mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, mradi utachangia katika kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi maeneo oevu na rasilimali za maji, kwa kutumia mbinu bunifu na shirikishi ambazo zitahakikisha ushiriki wa wananchi katika ulinzi na utunzaji wa mazingira yao.
IKI Katuma ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali ya Tanzania za kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa na mifumo ya ikolojia ya maeneo oevu zinatumika kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Utekelezaji wa mradi huu pia unaakisi dhamira ya dhati ya Serikali katika kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bioanuwai.