Habari

Imewekwa: Aug, 06 2020

Serikali Yatekeleza Ahadi ya Rais Magufuli Mbalizi

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWASA) kwa kutekeleza kwa haraka ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ya kufikishia huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya.

Ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea mradi wa Maji wa Shongo-Mbalizi katika Wilaya ya Mbeya Mjini ikiwa ni ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais Magufuli ya kuwaondolea kero ya ukosefu wa majisafi na salama wananchi wa Mbalizi aliyoitoa Aprili 27, 2019 kwa Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa.

Mhandisi Sanga amefurahishwa kuona ahadi ya Rais Magufuli kwa wananchi wa Mbalizi imetekelezwa, kwa mradi kufanya kazi na wananchi wameanza kunufaika kufuatia maelekezo aliyoyatoa wakati alipopita katika mji wa Mbalizi akiwa ziarani mkoani Mbeya ya kuhakikisha wananchi hao wanapata huduma ya majisafi na salama haraka.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo wa Sh. bilioni 3.3, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWASA), Mhandisi Ndele Mengo alisema ulianza kujengwa Julai 1, 2019 na kazi imefikia asilimia 98 na huku idadi ya wananchi waliounganishwa na huduma wamefikia 108 pamoja na vituo 10 vya kuchotea maji, ukiwa na uwezo kuzalisha kiasi cha lita milioni 10 kwa siku ukilinganisha na maji yanayotumika kwa sasa ya kiasi cha lita milioni nne kwa siku kutokana na maunganisho yaliyokwisha fanyika.

Mhandisi Sanga ameitaka Mbeya UWASA kuhakikisha inaongeza mtandao wa maji na kufikia wateja wengi zaidi, akisema ipo haja ya kuwafikia wananchi wengi zaidi kutokana na ukubwa wa mradi na kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Magufuli ya wananchi wote kufikiwa na huduma ya majisafi na salama.

Akizungumza mbele ya Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Usahandeshi, Joster Mwalingo alimshukuru Rais Magufuli kwa kutimiza ahadi yake kwa wananchi wa Mbalizi na kuipongeza Wizara ya Maji kwa kukamilisha haraka mradi huo kwa kuwa tangu kuanzishwa kwa kitongoji hicho kianzishwe hakijawahi kuwa na huduma ya maji.