Habari
Wizara ya Maji Yapewa Pongezi na Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira,
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeipongeza Wizara ya Maji kwa juhudi kubwa na kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Pamoja na pongezi hizo, Kamati imeitaka Wizara ya Maji kuongeza kasi ya utekelezaji na ukamilishaji wa miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.
Pongezi na maelekezo hayo yametolewa leo Januari 20, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Prof. Pius Yanda (Mb), kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Kamati hiyo pia imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Maji katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo Mpango Mkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji, ili kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa ufanisi katika maeneo ya mijini na vijijini.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema maelekezo na hoja zote zilizotolewa na Kamati zitafanyiwa kazi na wataalam ili kupata majibu ya kina, huku akisisitiza umuhimu wa watendaji wote kujituma na kuwajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi.
“Nawaomba watendaji wenzangu tukubali kubadilika ili Wizara yetu iweze kufanya vizuri zaidi. Huduma zetu ziendane na mahusiano mazuri na wananchi; naamini tunakwenda kujenga uhusiano imara zaidi,” amesema Mhe. Aweso.
Ameongeza kuwa Sekta ya Maji imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hata hivyo juhudi bado zinaendelea kuondoa changamoto ya uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo, hususan vijijini.
“Dhamira yetu ni kushirikiana kwa karibu na Kamati hii, kufanya kazi usiku na mchana, ili kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata huduma ya maji safi na salama,” ameainisha Mhe. Aweso.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhe. Mwajuma Waziri, pamoja na watendaji wa Wizara ya Maji na baadhi ya Mamlaka za Maji nchini.

