Habari

Imewekwa: Mar, 23 2022

Serikali Kuanza Utekelezaji wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda

News Images

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itatoa fedha za kuanza ujenzi wa Bwawa la Maji la Kidunda mkoani Morogoro ili kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama Jijini Dar es Salaam na mkoa wa Pwani.

Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia Siku ya Maji Duniani Kitaifa Jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City.

Rais Samia amesema mradi huo mkubwa utawezesha kuwepo kwa uhakika wa maji kwa kipindi chote mwaka mzima kwa Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani kwa kuwa kwa sasa mikoa hiyo inategemea maji ya Mto Ruvu ambayo asilimia 88 ya maji yote yanayozalishwa kwa ajili ya kuhudumia wakazi wake.

Rais Samia amesema kuwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira uliokithiri katika chanzo cha Mto Ruvu, kina cha maji cha mto huo kimekuwa kikipungua hasa wakati wa kiangazi hivyo mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kukosa kusukuma maji ya kutosha na kuleta changamoto ya huduma ya maji kwa wananchi.

Akisisitiza kuwa ujenzi wa bwawa hilo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2022 mpaka 2025 na utachochea kasi ya maendeleo ya viwanda katika mkoa wa Pwani pamoja na jiji la Dar es Salaam kwa kuhakikisha upatikanaji wa maji wakati wote mwaka mzima.

Aidha, Rais Samia amezindua Mfumo wa Pamoja wa Kusimamia Ankara za Maji (Unified Billing System) na Mfumo wa Taarifa za Miradi ya Maji (Maji App) iliyotengenezwa na wataalamu wa ndani, itakayoimarisha zaidi utoaji huduma ya maji kwa wananchi.

Pia, ametoa tuzo kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira zilizofanya vizuri kiutendaji Tanzania Bara kutokana na Ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA) kwa Mwaka 2020-2021.

Awali, Rais Samia alizindua Mradi wa Maji wa Mlandizi-Chalinze-Mboga katika Kata ya Msoga, mkoani Pwani wenye thamani ya Shilingi bilioni 19 ambao ujenzi wake ulisimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Baadhi ya maeneo yanayohudumiwa na mradi huu ni mji wa Chalinze na vitongoji vya Kata ya Msoga, Viwanda vya Tywford, Sayona, Kituo cha Treni ya Mwendokasi cha Kwala, Eneo la Mizani la Vigwaza pamoja na maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda.

Kaulimbiu ya Siku ya Maji Duniani mwaka 2022 ni Maji Chini ya Ardhi; Hazina Isiyoonekana kwa Maendeleo Endelevu, ikilenga kuonesha umuhimu wa rasimali maji zilizo chini ya ardhi katika usimamizi, uendelezaji na matumizi yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi na wananchi wake.