Habari

Imewekwa: Dec, 22 2025

RUWASA Kuzingatia Ubora wa Huduma na Uendelevu wa Miradi ya Maji

News Images

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Wolta Kirita, amesema taasisi hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha ubora na uendelevu wa huduma ya majisafi vijijini nchini vinazingatiwa.

Mhandisi Kirita amesema RUWASA imeanza rasmi ziara za ukaguzi katika wilaya za mikoa yote 25 ya Tanzania Bara ili kutathmini namna huduma ya maji inavyotolewa na Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) pamoja na uendelevu wa miradi ya maji.

Amesema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya majukumu ya kisheria ya RUWASA ya kusimamia na kudhibiti utendaji wa CBWSOs, pamoja na kutekeleza maelekezo ya viongozi wakuu wa Sekta ya Maji ya kuwataka viongozi kutoka ofisini na kwenda moja kwa moja kwenye maeneo ya huduma ili kujionea hali halisi ya utoaji huduma kwa wananchi na kutatua changamoto zinazojitokeza.

Mkurugenzi Mkuu Kirita amebainisha kuwa timu za Menejimenti ya RUWASA pamoja na wataalam wa Sekta ya Maji tayari zimeanza kazi hiyo katika mikoa mbalimbali nchini. kwa ushirikiano wa Mameneja wa RUWASA wa Mikoa na Wilaya, viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na viongozi wa CBWSOs husika.

Kwa upande wake, Meneja wa CBWSO, Vallentina Masanja, amesema kuwa hadi kufikia Novemba 2025, jumla ya CBWSOs 930 zilikuwa zinatoa na kusimamia huduma ya maji vijijini katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.

Ameeleza kuwa katika zoezi hilo, RUWASA itakagua maeneo muhimu ikiwemo usimamizi wa mapato na matumizi, taratibu za ununuzi, kiwango na muda wa huduma kwa siku, ubora wa maji, utunzaji na usimamizi wa miundombinu, utekelezaji wa hoja za ukaguzi pamoja na kufuatilia utekelezaji wa miongozo na maelekezo yanayotolewa na RUWASA na Serikali kwa ujumla katika utoaji wa huduma ya maji.

Zaidi ya CBWSOs 156 zinatarajiwa kufikiwa katika kipindi cha siku 10 za awali, huku ukaguzi huo ukiwa ni endelevu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Maji Na. 5 ya mwaka 2019, RUWASA ina jukumu la kusimamia, kudhibiti na kusaidia uendeshaji wa CBWSOs ili kuhakikisha wananchi wa maeneo ya vijijini wanapata huduma bora, salama na endelevu ya majsafi.