Habari

Imewekwa: May, 05 2020

RUWASA, DUWASA zatakiwa Kupanua Wigo wa Huduma ya Maji

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Dodoma; 05 Mei, 2020

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kupanua wigo wa huduma kwa wananchi na kutimiza lengo la kuanzishwa kwa taasisi hizo.

Ametoa rai wakati akizungumza na menejimenti ya taasisi hizo kwa nyakati tofauti akisisitiza watumishi kutobweteka na mafanikio waliyoyapata, zaidi wanatakiwa kudhamiria kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wengi zaidi.

Naibu Waziri Aweso ameitaka RUWASA kuimarisha utaratibu wa manunuzi, ili kuondoa vikwazo katika kukamilisha miradi ya maji kwa wakati na sio kwa utaratibu wa zamani ulioigharimu wizara kwa kiasi kikubwa.

Akisema amefurahishwa na taarifa ya Mtendaji Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Clement Kivegalo kukikiri changamoto hiyo na kuchukua hatua, wakiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kisheria za kuwa mfumo mmoja wa manunuzi ya RUWASA kwa nchi nzima ili kuondoa vikwazo mbalimbali na kukamilisha miradi kwa wakati.

Akisisitiza umuhimu wa RUWASA ni upatikanaji wa maji bombani katika vijiji vyote nchini, na kuitolea mfano miradi ya maji ya Nyamtukuza katika Wilaya ya Nywang’hwale, mkoani Geita na Mwakitolyo katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini mkoani Shinyangailiyokuwa imekwama kwa muda mrefu na sasa ipo katika hatua nzuri kama moja ya mafanikio ya RUWASA.

Awali, Naibu Waziri Aweso ameilekeza DUWASA kuongeza nguvu katika maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Dodoma ili kuhakisha wakazi wote wa maeneo hayo wanafikiwa na huduma ya maji ya uhakika, ili kuendana na ongezeko la mahitaji yanayotokana na kasi ya ukuaji wa jiji hilo.

Akitoa taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David Pallangyo amesema wamejipanga kutoa maji katika Ziwa Victoria kama suluhisho la muda mrefu, lakini pia kutumia vyanzo vya visima vilivyopo kwenye mji wa Chamwino vyenye uwezo wa kutoa maji kwa miaka mitano ijayo kufikisha huduma kwenye maeneo ya pembezoni mwa jiji kama suluhisho la muda mfupi.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini