Habari

Imewekwa: Jan, 26 2026

Wawekezaji Kutoka China na Wizara ya Maji Wajadili Kuhusu Dira za Maji za Malipo ya Kabla

News Images

Kampuni ya Flowmovement Technology kutoka nchini China imeanza mazungumzo na Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa lengo la kuwekeza nchini katika Sekta ya Maji, hususan kwenye uzalishaji na matumizi ya dira za maji za malipo ya kabla (pre-paid meters) ili kuboresha na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Mazungumzo hayo yameongozwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uendeshaji na Matengenezo Wizara ya Maji, Mhandisi Mashaka Sitta, pamoja na viongozi wengine wa Wizara katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Maji jijini Dodoma.

Mbali na utengenezaji wa dira za maji za malipo ya kabla, kampuni hiyo imeeleza nia yake ya kuwekeza nchini kwa kufungua kiwanda cha kutengeneza dira hizo, kufanya tafiti za kubaini vyanzo vya maji, kupunguza upotevu wa maji na kuongeza ufanisi katika usambazaji wa maji nchini.

Mhandisi Sitta amesema nia ya kampuni hiyo kuwekeza nchini inaendana na mahitaji ya sasa ya Sekta ya Maji, huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, endelevu na kwa viwango vinavyokubalika.

Aidha, Serikali imesisitiza umuhimu wa dira za malipo ya kabla zitakazo zingatia mazingira halisi ya Tanzania kutokana na tofauti za hali ya hewa na upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Vilevile, kabla ya kuanza rasmi kwa matumizi ya dira hizo, Serikali inapanga kuweka mikakati madhubuti ikiwemo upatikanaji wa dira hizo kwa gharama nafuu, zenye matengenezo rafiki, kuwa bei elekezi ya huduma ya maji ili wananchi wote waweze kunufaika pamoja na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Mhandisi Sitta amewashukuru wawekezaji hao kwa kuonesha nia ya kuwekeza nchini na kuwataka kuendelea kubuni teknolojia zitakazoendana na mazingira ya Tanzania.