Habari

Imewekwa: Sep, 17 2023

Rais Samia awapa Mtwara uhakika wa maji

News Images

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Mtwara kuwa serikali inaendelea na jitihada mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wote wa mkoa huo wanafikiwa na huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.


Rais Samia ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Newala katika uwanja wa Sabasaba mara baada ya kutembelea banda la Wizara ya Maji na kupata maelezo kuhusu mradi wa maji wa Makonde kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri.

Amesema mradi wa maji wa Makonde unaotekekezwa mkoani hapo utahudumia sehemu kubwa ya wananchi na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya huduma ya majisafi.

Mhe. Rais Amewapongeza wizara ya Maji kwa kuendelea kusimamia ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Kabla ya kuwasili wilayani Newala akitokea Mtwara mjini, Mhe. Rais Samia alisimama na kuzungumza na wananchi wa eneo la Nanguruwe, wilaya ya Mtwara, Jimbo la Mtwara Vijijini.

Katika mkutano huo Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) alipata fursa ya kuzungumza na wananchi na kuwahakikishia kuwa serikali imejipanga kwa mipango mizuri ili wananchi wa mkoa wa Mtwara ikiwemo jimbo la Mtwara Vijijini kunufaika na majisafi na salama yenye kutosheleza.

Mipango hiyo ni pamoja na kuhakikisha unatekekezwa mradi mkubwa utakaotumia chanzo cha mto Ruvuma ili kuhudumia maeneo mbalimbali mkoani hapo.