Habari

Imewekwa: Mar, 21 2022

Rais Mhe. Samia Mgeni Rasmi Siku ya Maji Duniani Kitaifa, 22 Machi, 2022

News Images

Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Maji Duniani itakayofanyika kitaifa Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Machi, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City.

Tanzania itaungana na nchi nyingine kuadhimisha Siku ya Maji Duniani inayotokana na Azimio Na. 47/193 la Umoja wa Mataifa (UN) kuwa kila tarehe 22 Machi ya kila mwaka, nchi wanachama ziadhimishe Siku ya Maji Duniani kwa pamoja ikiwa ni kutambua umuhimu na thamani ya maji katika maisha ya binadamu na uchumi wa dunia kwa ujumla.

Kaulimbiu ya maadhimisho haya Mwaka huuni Maji Chini ya Ardhi; Hazina Isiyoonekana kwa Maendeleo Endelevu, ujumbe huu unalenga kuonesha umuhimu wa rasimali maji zilizo chini ya ardhi katika usimamizi, uendelezaji na matumizi yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi kwa manufaa ya wananchi na mazingira kwa ujumla.

Kitaifa, hapa nchini Siku ya Maji Duniani hutanguliwa na Wiki ya Maji inayoanza kila mwaka tarehe 16 - 22, Machi kwa shughuli mbalimbali; ikiwa ni pamoja na uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi ya maji. Hiki ndicho kipindi ambapo wananchi na wadau huoneshwa kazi mbalimbali zilizofanyika katika Sekta ya Maji pamoja na kupewa jukwaa la kutoa sauti zao kuhusu huduma ya maji.

Mwaka huu 2022, Wiki ya Maji ilizinduliwa tarehe 15 Machi, 2022 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango kwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Orkesumet wenye thamani ya Sh. bilioni 41.5. Uzinduzi huo ulifanyika wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.

Mhe. Rais Samia, pamoja na kuwa Mgeni Rasmi anatarajiwa kushiriki katika matukio yafuatayo;

Mosi, atazindua Mradi wa Maji wa Mlandizi- Chalinze - Mboga wenye thamani ya Sh. bilioni 19, na mradi huu unanufaisha takribani wananchi wapatao 120,000.

Uzinduzi utafanyika katika Kata ya Msoga, Mkoani Pwani. Mradi huu unahudumia maeneo ya Mji wa Chalinze na vitongoji vya Kata ya Msoga, Viwanda vya Tywford, Sayona, Kituo cha Treni ya Mwendokasi

cha Kwala, Eneo la Mizani la Vigwaza pamoja na maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

Uzinduzi wa Mradi wa Maji wa Mlandizi-Chalinze-Mboga utaanza saa 02:00 asubuhi na wananchi wote wanakaribishwa, hakuna kiingilio.

Aidha, katika eneo la Mlimani City, ambapo Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani yatafanyika kuanzia saa 6 mchana, kutakuwa na maonesho ya bidhaa na huduma tofauti tofauti zinazohusiana na huduma ya maji kutoka kwa Taasisi za Serikali na Binafsi, Kampuni na Viwanda mbalimbali vya hapa nchini.

Maadhimisho yanatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 2,500 wakiwamo, viongozi mbalimbali wa Serikali, Mabalozi, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi.

Mkutano Mlimani City utaanza saa 6.00 mchana.