Habari

Imewekwa: Jan, 12 2026

​Naibu Waziri Maji awapa kongole Mwanza

News Images

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo mathew amehitimisha ziara yake mkoani Mwanza na kuwapongeza watendaji wa sekta ya maji mkoani hapo kwa usimamizi mzuri wa miradi inayoendelea.

Ametembelea mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji kutoka mradi ambao chanzo chake ni Butimba jijini Mwanza, Mradi wa ujenzi wa tenki la lita milioni tano Nyamazugo pamoja na ule wa Kijiji cha sima vyote vya wilayani Sengerema.

Amesisitiza kuwa agizo la serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha sekta ya maji inapata ufumbuzi wa changamoto zinazoikumba kwa haraka ili kuwezesha huduma ya maji kuwafikia watanzania wote. Amesema ufumbuzi huo ni pamoja na kuanza kutumia dira za maji za malipo kabla zitakazowezesha kuondoa malalamiko ya bili za maji na kuwezesha malipo ya haraka kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi.

Amewaagiza viongozi wa sekta ya maji mkoani hapo kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuhakikisha wateja wote wanatumia dira za maji za malipo kabla.

Ameongeza kuwa serikali inaendelea na hatua ya utekelezaji wa ujenzi wa Gridi ya Maji ya Taifa ambayo hatua zake ni pamoja na kutumia vyanzo vya uhakika vya maji ukiwemo mradi wa maji wa Butimba ambao unaigusa sehemu kubwa ya jiji la Mwanza ukitumia chanzo cha maji ya ziwa Victoria.

Pia amewahakikishia wakandarasi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia imejipanga na haitakwama kwa njia yoyote katika jitihada zake za kumtua mwanamke wa Kitanzania ndoo ya maji kichwani.