Habari

Imewekwa: Mar, 13 2023

​Mradi wa Maji Same -Mwanga-Korogwe kukamilika Ndani ya miezi 14.

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewataka wakandarasi wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe kukamilisha kazi zilizosalia katika mradi huo ndani ya miezi 14 kuanzia Machi 2023.

Ametamka hayo wilayani Mwanga wakati wa kusaini makubaliano ya kuhuisha mkataba kati ya Wizara ya Maji na mkandarasi kampuni ya M.A. Kharif & Sons kuhusu kukamilisha ujenzi wa mradi huo.

"Baada ya dhiki ni faraja, na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha za kutosha kumaliza kazi hii" Mhe. Aweso amesema na kusisitiza mkandarasi asiweke sababu zozote za kukwama mradi

Amesema wananchi wamesubiri sana maji, sasa ndani ya miezi 14 lazima wapate majisafi, salama na toshelevu.

Amesema viongozi wa Wizara watafanya kazi usiku na mchana, na kumwelekeza mkandarasi kuweka ratiba ya mpango kazi hadi kukamilisha mradi.

Akiongea kuhusu kazi zilizobaki, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesema ni pamoja na kazi ya ulazaji mabomba ambayo yameshafika na kazi inaendelea.

Amesema pia, kuweka mfumo wa umeme ili kusukuma maji kwenda katika matanki, ambapo mradi una idadi ya matanki saba ya kuhudumia wananchi.

Hafla hiyo imehudhuria na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Nurdin Babu ambaye amewataka wananchi kushiriki katika miradi ya maji kwa kulinda vyanzo vya maji.