Habari

Imewekwa: Mar, 23 2023

​Mkopo nafuu kuimarisha Mamlaka za Maji – Mha. Luhemeja

News Images

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja amezitaka mamlaka za maji nchini kuweka malengo ya makusanyo ili kuona thamani ya kuongeza mtandao wa huduma na idadi ya wateja kupitia mkopo nafuu.

Mhandisi Luhemeja amesema hayo jijini Dar es salaam wakati wa kikao cha kujenga uelewa kuhusu utaratibu uliowekwa kwa mamlaka za maji kuomba mikopo nafuu ya utekelezaji wa miradi ya maji kupitia dirisha la Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF).

“Huu mfuko lazima uangalie namna ya kuisaidia sekta ya maji kuimarika zaidi, na kwa hili nawapongeza sana kwa sababu kila mamlaka ya maji itakuwa na wasaa wa kujiimarisha zaidi kupitia mkopo” Mhandisi Luhemeja amesema na kuongeza kuwa kila mamlaka lazima ipambane kuongeza matokeo ya kazi na kuweka malengo ya makusanyo.

Ameongeza kuwa dirisha la mikopo ni sehemu ya kuongeza mapato katika mamlaka za maji na hatua hiyo itazifanya mamlaka zijipange kukua na kujitegemea.

Mhandisi Luhemeja amesisitiza mikopo irudishwe kuendana na makubaliano yaliyowekwa na sio vinginevyo ambapo riba yake ni asilimia sita.

Ameongeza upo umuhimu wa kukitumia Chuo cha Maji ambacho ni sehemu ya wizara katika kazi mbalimbali za sekta ya maji ikiwamo mafunzo ili kukipa thamani zaidi, pia utunzaji wa rasilimaliza maji ili kuepuka uharibifu na uhaba wa huduma za maji.

Mhandisi Luhemeja ameainisha kuwa mwendo na malengo kwa kila eneo ni upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi kufika asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini, hivyo kila mamlaka ijipime hadi sasa ilipofika.

Moja ya majukumu ya Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) ni kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kusaidia uwekezaji kwenye miradi ya majisafi na miradi ya utunzaji wa vyanzo vya maji, na utoaji wa mikopo utaongozwa na Mwongozo wa Mfuko wa Utoaji Mikopo wa Mwaka 2022.

Kitengo cha Mawasiliano