Habari

Imewekwa: May, 05 2026

Wizara ya Maji Yaja na Vipaumbele Mahsusi Mwaka 2026/2027

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amewasilisha bajeti ya takriban shilingi trilioni 1.12 yenye vipaumbele mahususi kwa Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akitoa matumaini mapya kwa mamilioni ya Watanzania wanaosubiri kuboreshwa kwa huduma ya majisafi na salama.

Akiwasilisha hotuba yake Bungeni jijini Dodoma, Waziri Aweso amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji ili kuhakikisha usalama wa maji na upatikanaji wake kwa shughuli za kijamii, kiuchumi na ikolojia.

“Kwa mwaka 2026/2027, Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji kwa lengo la kuhakikisha usalama wa maji na upatikanaji wake kwa shughuli za kijamii, kiuchumi pamoja na ikolojia,” amesema Aweso.

Waziri ametaja vipaumbele mahususi vitakavyotekelezwa katika mwaka huo wa fedha. Kwanza, Wizara itakamilisha maandalizi ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji (National Water Master Plan) pamoja na kuendeleza utekelezaji wa miradi ya Gridi ya Taifa ya Maji. Mradi huo unalenga kutumia vyanzo vya uhakika kama maziwa na mito kupeleka maji katika maeneo yenye uhaba mkubwa.

Pia, katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukame, Wizara itaweka mkazo katika uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua. Katika mwaka huo, imepanga kujenga na kukarabati mabwawa 33, kubuni mabwawa mapya 34, na kufanya tathmini ya athari za kimazingira kwa mabwawa mawili. Aidha, wananchi watahamasishwa kuvuna maji ya mvua kupitia mapaa ya nyumba ili kuongeza uhakika wa maji katika maeneo yenye changamoto.

Katika kuharakisha upatikanaji wa huduma, Wizara itaweka msukumo wa kukamilisha miradi inayoendelea. Imepanga kukamilisha miradi 992 ya majisafi vijijini, miradi 196 ya majisafi mijini, na miradi 26 ya usafi wa mazingira.

Aidha, katika mwaka 2026/2027, Wizara itaanza utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 314 kati ya vijiji 1,575 ambavyo bado havina huduma ya majisafi. Hatua hii inalenga kuwafikia wananchi waliosalia nyuma katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Waziri Aweso ameweka mkazo pia katika kudhibiti upotevu wa maji ambao ni changamoto kubwa katika sekta hiyo. Amesema Wizara itatumia teknolojia za kisasa zikiwemo mifumo ya usomaji mita kielektroniki, ufuatiliaji wa mtandao wa maji (smart water management system), ukarabati wa miundombinu na ufungaji wa mita za malipo ya kabla. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanaoharibu miundombinu na wanaojihusisha na wizi wa maji.

Msisitizo maalum umetolewa kuhakikisha shule na vituo vya afya vinapata huduma ya majisafi na usafi wa mazingira. Wizara itashirikiana kwa karibu na wizara nyingine, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na wadau mbalimbali ili kuhakikisha taasisi muhimu za umma zinapata maji ya uhakika.

Kufanikisha vipaumbele hivyo, Wizara imepanga kutumia vyanzo mbadala vya fedha ikiwemo Hati Fungani (Bonds), kuhamasisha wawekezaji wa sekta binafsi, kutumia fedha za mifuko ya mabadiliko ya tabianchi, na kuimarisha Mfuko wa Taifa wa Maji ili uweze kupata ufadhili kutoka taasisi za kimataifa. Pia itaimarisha mifumo ya TEHAMA, kuendeleza rasilimali watu, kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya miradi.

Bajeti ya Wizara ya Maji inakuja wakati Serikali inaendelea kutekeleza ahadi yake ya kuhakikisha wananchi wanapata majisafi, salama na ya kutosha kama msingi wa maendeleo ya jamii na chachu ya kujenga uchumi wa Tanzania.